OHIO, MAREKANI
BINGWA wa mchezo wa tenisi nchini Hispania, Rafael Nadal, wiki ijayo anatarajia kushika nafasi ya kwanza kwa ubora wa nchini humo duniani akichukua kutoka kwa Andy Murray aliyeshindwa kushiriki michuano ya Cincinnati Master.
Murray ameshindwa kushiriki michuano hiyo kutokana na kusumbuliwa na kiwiko cha mkono, hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwa kuwa anatarajia kufanyiwa upasuaji.
Nafasi hiyo ya kwanza kwa ubora inawaniwa na Nadal pamoja na Roger Federer, lakini Federer ametangaza kutoshiriki Western na Southern katika michuano ya Cincinnati Master kutokana na majeruhi, hivyo Nadal atakuwa na nafasi hiyo ya kupaa katika viwango vya tenisi duniani endapo atafanya vizuri.
Federer amewahi kushika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani kwa kipindi cha miaka minne kati ya 2004 hadi 2008, baada ya hapo alikuwa anakutana na ushindani wa hali ya juu kutoka kwa wapinzani wake hasa katika michuano ya Rogers Cup.
Federer ametumia akaunti yake ya Twitter kuwaomba radhi mashabiki wake ambao walitarajia kumuona kwenye michuano hiyo ya Cincinnati Master.
“Kwa masikitiko ni kwamba mashabiki wangu walikuwa na lengo la kuniona kwenye michuano ya Cincinnati, lakini nataka kuwaambia kwamba ninahitaji kupumzika.
“Nilipambana kuhakikisha ninafanya vizuri kwenye michuano ya Rodger Cup, lakini sikuweza kufanikiwa mbele ya mpinzani wangu, Alexander Zverev, hivyo kwa sasa natakiwa kupumzika ili kujiweka sawa kwa ajili ya michuano mingine, nawaomba radhi mashabiki zangu,” aliandika Federer.
Orodha ya wachezaji bora wa tenisi kwa sasa inashikwa na Andy Murray nafasi ya kwanza, huku nafasi ya pili ikishikwa na Rafael Nadal, nafasi ya tatu Roger Federer, nafasi ya nne Stan Wawrinka na nafasi ya tano ikichukuliwa na Novak Djokovic.