SHA KIGUNDULA, SHINYANGA
SIMBA wameshindwa kutimiza azma yao ya kumaliza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL 2019/20) bila kupoteza mchezo baada ya jana kufungwa bao 1-0 na Mwadui Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini hapa.
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza kati ya saba waliyoshuka dimbani, ikiwa ni baada ya kushinda sita mfululizo.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, bado Simba wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 18 walizozivuna ndani ya mechi saba, wakifuatiwa na Kagera Sugar wenye pointi 16 kutokana na mechi nane, wakifungana pointi na Namungo wanaofuatia waliocheza mechi tisa.
Kwa upande wao, kwa ushindi wa jana, Mwadui wamechupa kutoka nafasi ya 12 hadi ya nane, wakiwa wamejikusanyia pointi 11 kutokana na mechi tisa.
Alikuwa ni Gerald Mathias aliyeifungia Mwadui bao pekee katika mchezo huo wa jana, akifanya hivyo kwa kichwa dakika ya 32 akiwa ndani ya 18 na kumwacha kipa wa Simba, Aishi Manula, akiwa amelala chini.
Kwa ujumla, mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo Simba walionekana kupania kuwachanganya wenyeji wao kwa bao la mapema na alikuwa ni kiungo wao, Sharaf Shiboub, aliliyelitia majaribuni lango la Mwadui kwa kuachia shuti kali akiwa nje ya 18, lakini mpira ulipita pembeni ya goli.
Simba waliendeleza mashambulizi kwenye lango la Mwadui ambapo dakika ya 19, Mzamiru Yassin aliyepokea pasi ya Clatous Chama, alikosa bao baada ya kuachia shuti kali na mpira kupita pembeni ya goli.
Meddie Kagere almanusura awainue mashabiki wa Simba katika dakika ya 20 baada ya kuachia mkwaju akiwa eneo hatari, lakini mpira ulipaa.
Katika dakika ya 32, Mathias aliwainua mashabiki wa Mwadui kwa bao lake hilo lililoonekana kuwapa nguvu Mwadui, huku Simba wakihaha kutaka kusawazisha na kuongeza lingine kama si mengine.
Mathias nusura aifungie Mwadui bao la pili katika dakika ya 43 baada ya kupiga shuti kali akiwa nje kidogo ya 18, lakini kipa wa Simba, Manula aliweza kuokoa hatari hiyo.
Ikiwa imebaki dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko, Shiboub alikaribia kuwainua mashabiki wa Simba pale alipopiga ‘tick tack’ akiwa ndani ya 18, lakini mpira ulipita pembeni ya goli.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Mwadui wakionekana kuwa moto zaidi ambapo Hassan Kapalata almanusura aipatie timu yake hiyo bao la pili baada ya kuachia shuti na mpira kupita pembeni.
Dakika ya 76, Ibrahim Ajib wa Simba aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Francis Kahata, alipiga mpira wa faulo na kupita juu kidogo ya lango la Mwadui.
Katika dakika ya 86, Yassin alikaribia kuwainua mashabiki wa Simba baada ya kupiga mpira wa kichwa akiwa katikati ya mabeki wa Mwadui, lakini mpira ulipita pembeni ya goli, akiunganisha krosi murua kutoka kwa Ajib.
Dakika 90 zilimalizika huku Mwadui FC wakitoka kifua mbele baada ya kuikalisha Simba kwa kuifunga bao 1-0.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, Mtibwa Sugar ikiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, iliifumua Coastal Union mabao 2-1, KMC ikionjeshwa joto ya jiwe na Ruvu Shootingi kwa kuchapwa bao 1-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Mjini Iringa, Lipuli FC iliishushia Polisi Tanzania kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Samora, huku Kagera Sugar wakiwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, wakitakata kwa kuichabanga Namungo mabao 2-0.
Nao JKT Tanzania, wakiwa ugenini, walivuna ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.