Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimesikitishwa na kitendo kilichofanywa na muhudumu wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, aliyedaiwa kumchomoa mgonjwa dripu ya maji na kumuuzia mwengine kwa Sh 5000.
Kwa mujibu wa Rais wa chama hicho, Paul Magesa, alisema inasikitisha kitendo alichofanya muhudumu huyo ambacho pia ni ukatili.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Magesa alisema neno lililotumika kwa kumwita muuguzi wakati hakuwa muuguzi kwa taaluma ni makosa makubwa.
Magesa ametaka waombwe radhi kwa kuchafuliwa.
“Siyo muuguzi kama ambavyo imeripotiwa, yeye ni muhudumu wa afya … muuguzi ni yule aliyesomea fani ya uuguzi na kupewa cheti akatambulika.
“Yeye tumefuatilia baada ya taarifa hiyo… tumesikitika sana kutumiwa neno muuguzi.
“Yeye ni muhudumu tu na kazi za wahudumu wa afya katika hospitali au zahanati husika ni kufanya usafi wodini, kupeleka vipimo maabara, kumpeleka mgonjwa,” alisema Magesa.
Alisisitiza haja ya serikali kuona umuhimu wa kuajiri wauguzi wengi hasa maeneo ya pembezoni mwa nchi kuepuka kadhia kama hizo zilizotokea na kuharibiwa jina lao la taaluma na kuchafuliwa katika jamii.
Alisema baraza litaendelea kufanya uchunguzi kugundua kama kuna wahudumu wengine wanafanya kazi zao kinyume na taratibu ya taaluma waliyopata vinginenvyo watawaingiza kwenye matatizo na jamii kwa kujua wote ni wauguzi.
Juzi, gazeti moja la kila siku (si Mtanzania), liliripoti habari hiyo huku Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Tunduru kukiri kupata taarifa za kutokea tukio hilo na kupeleka taarifa kwa mganga mkuu wa wilaya kwa hatua zaidi.