23.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 2, 2024

Contact us: [email protected]

Muhas yaonya matumizi holela ya dawa kwa wajawazito

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imeshauriwa kuweka msisitizo kuzuia matumizi ya dawa kiholela kwa wajawazito ili kuepusha madhara kwani zikitumika kwa muda mrefu husababisha ufubavu.

Hatua hiyo inafuatia baada ya utafiti uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kubaini wajawazito wengi wanatumia dawa kwa kiasi kikubwa.

Dk. Edward Mhina ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tat katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), amewasilisha utafiti huo Juni 27,2024 wakati wa kongamano la 12 la kisayasi la chuo hicho.

Amesema alifanya utafiti huo kuangalia matumizi ya dawa wakati wa wajawazito kwa lengo la kubaini sababu zinazochangia hali hiyo.

“Nimegundua kulikuwa na sababu kubwa mbili; kuna sababu za kimazingira ambapo wajawazito waliokuwa wanakaa mbali na vituo vya afya walikuwa na urahisi wa kutumia dawa bila kumuona daktari.

“Sababu nyingine ya kimazingira ilionyesha kwamba mjamzito akienda hospitali na akikaa kwa muda mrefu kusubiri kupata huduma kutoka kwa daktari inamfanya wakati mwingine kuamua kutumia dawa pasipo kumuona daktari…wengine wanaona uvivu kwenda hospitali,” amesema Dk. Mhina.

Amesema matumizi ya dawa wakati wa ujauzito yanaweza kuibua vitu mbalimbali kwa wajawazito kama vile kujifungua watoto njiti, kusababisha ufubavu wa dawa na nyingine.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, akizungumza wakati wa kongamano la 12 la kisayansi la chuo hicho Dar es Salaam.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema baadhi ya tafiti zilizofanywa na chuo zimesaidia kubadilisha sera, kuleta miongozo ya matibabu ya magonjwa, kuimarisha huduma za afya.

“Kongamano linalenga kusambaza matokeo ya tafiti za afya nchini hivyo ni wakati wa kutafakari mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia tafiti kwa ajili ya kuboresha jamii yetu,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Aidha amesema utekelezaji wa ndoto ya kuwa na vituo vya umahiri katika maeneo mbalimbali unaanza, awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu maaandalizi yamekamilika na mipango ya kuanzisha hospitali ya moyo tayari imeanza.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amevitaka vyuo vikuu kufanya tafiti zinazotoa majibu kwa changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii.

“Makongamano kama haya ni muhimu sana kuja kuonyesha nini tumetafiti na matokeo yake yanaweza yakatumika namna gani katika maisha ya kila siku. Yanasaidia kuweka nchi yetu katika ramani ya dunia ya kisayansi na kuboresha mbinu mbalimbali za kufanya kazi,” amesema Profesa Nombo.

Kongamano hilo pia limetumika kumuenzi aliyekuwa mkuu wa kwanza wa chuo hicho Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi kutambua mchango wake hasa katika upanuaji wa miundombinu ya kufundishia, kutoa huduma na tafiti ikiwemo uanzishwaji wa Kampasi ya Mloganzila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles