HARARE, ZIMBABWE
RAIS wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe jana alishindwa kujitokeza mbele ya Bunge la Zimbabwe alikoitwa kutoa ushahidi kuhusu rushwa katika tasnia ya madini ya almasi.
Mugabe (94) ambaye amedhoofu kiafya, alitakiwa kufika saa tatu asuhubi lakini hakujitokeza na kuwafanya wabunge wapange upya siku ya kumuita kuwa ni Jumatatu ijayo.
Kamati inayoongozwa na Temba Mliswa, mbunge wa kujitegemea, iliwaambia wanahabari kwamba kamati ya Bunge ilitambua kwamba saa tatu asubuhi ni mapema mno kwa rais huyo wa zamani kujitokeza.
Alisema kwamba kikao cha Jumatatu ijayo kimefanywa saa nane mchana, ingawa hakuna uthubitisho wowote kutoka ofisi ya Mugabe wa kuhudhuria.
Wabunge wanataka kumhoji Mugabe kuhusu madai yake ya mwaka 2016 kwamba Zimbabwe ilipoteza mapato ya dola bilioni 15 kutokana na rushwa na unyonyaji wa kigeni katika sekta ya almasi.
“Hatupo hapa kumdhalilisha, tunatarajia awe na muda wa kutosha kujiandaa. Hivyo Jumatatu saa 8.00 mchana tunamtarajia hapa,” Mliswa alisema, akikiri kwamba Mugabe halazimishwi kisheria kuhudhuria.
Mugabe aliitawala Zimbabwe kuanzia mwaka 1980 hadi alipong’olewa madarakani Novemba mwaka jana kufuatia utwaaji madaraka uliofanywa na jeshi kwa muda mfupi.
Alilaani kung’olewa kwake kuwa ni mapinduzi na hajaonekana hadharani tangu siku hiyo.
Hata hivyo, utawala wake wa kiimla ulituhumiwa kujinufaisha na faida inayotokana na almasi.
Nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa naibu wake na mfuasi mtiifu kabla hawajafarakana, Emmerson Mnangagwa ambaye aliungwa mkono na maofisa waandamizi wa jeshi.
Zimbabwe iligundua utajiri wa almasi huko Chiadzwa, mashariki mwa nchi miaka zidi ya 10 iliyopita.
Makundi ya haki za binadamu yametuhumu vyombo vya usalama kutumia njia za kikatili kudhibiti utajiri huo.
Kamati ya Bunge, tayari imewahoji mawaziri wa zamani na wakuu wa usalama kuhusu sekta ya madini Chiadzwa.
Julai mwaka huu, Zimbabwe itafanya uchaguzi wa kwanza bila Mugabe huku chama tawala cha Zanu-PF kikitabiriwa kubaki madarakani.