CAIRO, MISRI
RAIS wa Misri, Abdel-Fatah al-Sisi ametangaza miezi mitatu ya hali ya hatari kutokana na mashambulizi mawili ya mabomu ya kujitoa mhanga yaliyofanywa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).
Milipuko hiyo iliua watu 49 katika maadhimisho ya Jumapili ya Mitende, yakiwa ni mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya Wakristo walio wachache nchini hapa katika siku za karibuni.
Mashambulizi hayo yaliyotokea katika miji ya jimbo la Nile Delta ya Tanta na Alexandria yalifuatia shambulizi la kanisa moja mjini Cairo Desemba 2016.
Aidha yalikuja wiki chache kabla ya ziara ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis inayonuia kuonyesha mshikamano na jamii ya Wakristo wa hapa.
Rais Sisi ametangaza amri hiyo, ambayo atapaswa kuiwasilisha bungeni ndani ya wiki moja.
“Hatua kadhaa zitachukuliwa, kwanza ni kutangaza hali ya hatari baada ya kukamilika taratibu zinazofaa kisheria na kikatiba kwa miezi mitatu nchini Misri.”
“Tunatangaza hali hii ya hatari kwa kuilinda nchi yetu tu na kuzuia kuingiliwa kwa njia yoyote,” taarifa ya ofisi ya rais ilisema.
Papa Francis ambaye anatarajiwa kuzuru Misri Aprili 28 na 29, aliwaombea waathirika wa mashambulizi hayo.
“Ninawaombea waliokufa na waliojeruhiwa. Mungu aibadilishe mioyo ya wale wanaoeneza ugaidi, machafuko na kusababisha vifo, na pia mioyo ya wale wanaotengeneza na kuingiza silaha”.
Wapiganaji wa itikadi kali wanawatuhumu Wakristo wa madhehebu ya Coptic kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani Rais kutoka kundi la Muslim Brotherhood, Mohamed Morsi mwaka 2013.
Wacoptic ambao wataadhimisha Pasaka wiki ijayo, wamekuwa wakilengwa na mashambulizi kadhaa katika miezi ya karibuni.