Anna Ruhasha, GeitaÂ
Kampuni ya Mgodi wa Buckreef imetenga Sh milioni 321 kwa ajili ya maendeleo ya jamii hususan nyanja ya elimu, afya na maji lengo likiwa ni kupunguza changamoto zinazowakabili wakazi wa Halmshauri ya Wilaya ya Geita vijijini mkoani humo.
Akizungumza leo Septemba 18, mbele ya mbunge wa Geita mjini, Costantine Kanyasu alipotembelea banda hilo, Meneja Rasilimali watu wa Mgodi wa Buckreef, Amerida Msuya, amesema wamejikita kusaidia jamii inayowazunguka kwa kuboresha huduma muhimu.
Msuya amesema kuwa mgodi wa Buckreef ambao unamilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inayomiliki asilimia 45 na mbia ambaye ni Tanzamu 200, inayomiliki asilimia 55, amesema wametenga Dola milioni 74 kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa kisasa.
“Lakini wakati tunaendelea na ujenzi wa mgodi tayari tunatoa huduma kwa jamii mfano mpaka sasa tumejenga vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Tembo na tumekabidhi madawati katika shule ya Sekondari ya Kasem,” amesema Msuya.
Upande wake, Mbunge Kanyasu amesema kilio cha wananchi na serikali ni kuona uwekezaji huo unajitoa zaidi katika kutekeleza shughuli za kijamii kama sheria inavyoelekeza ambapo pia amepongeza kuona tayari wameanza toa mchango kwenye jamii inayowazunguka.