Na LILIAN JUSTICE-MOROGORO
MGANGA Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, amesema Mkoa wa Morogoro umeendelea kusimamia vizuri suala la afya kinga kwa jamii, ikiwamo kuhamasisha jamii kuwa na vyoo bora ili kujikinga na maradhi.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake juzi, Dk. Jacob alisema wao kama mkoa, wameweza kusimamia vizuri suala la afya kinga kwa jamii ili kuweza kufikia asilimia 90 katika kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora.
Dk. Jacob alisema kuwa, bado kuna kaya ambazo hazina vyoo bora, jambo ambalo ni la hatari kwa kuwa kuna uwezekano wa kuwapo kwa magonjwa ya milipuko.
“Naihamasisha jamii, hususan kila kaya kuhakikisha inakuwa na choo bora na kuweka mazingira safi yanayowazunguka ili kujiepusha na mlipuko wa magonjwa yatokanayo na uchafu, ikiwamo kuhara na kipindupindu.
“Kwa wale wasiokuwa na vyoo, lazima waelewe kwamba vyoo ni muhimu katika maisha, kwa sababu vinaepusha mambo mengi, yakiwamo magonjwa yanayoweza kuepukika.
“Pamoja na hospitali ya mkoa kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wagonjwa, bado tunakabiliwa na changamoto ya kuwa na mrundikano wa wagonjwa.
“Kwa hiyo, moja ya mikakati yetu hapa hospitalini ni kujenga wodi katika Kituo cha Afya Sabasaba, ili kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika hospitali yetu ya mkoa,” alisema Dk. Jacob.
Kwa upande wake, Mkazi wa Sabasaba, Manispaa ya Morogoro, Zuwena Issa, alisema ujenzi wa wodi katika Kituo cha Afya Sabasaba, utawapunguzia kero ya kupata huduma za afya ambayo wamekuwa wakiipata kila wanapohitaji kutibiwa.