NA PETER FABIAN, MWANZA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, amesema mfungwa mmoja na mahabusu wawili wameuawa baada ya kutoroka gereza kuu la Butimba jijini Mwanza.
Alisema mahabusu hao, walifariki dunia wakiwa hospitali baada ya kipigo cha wananchi waliowakamata huku mfungwa akifariki baada ya kupigwa risasi na askari alipojaribu kutoroka alipokuwa akienda kuonyesha dereva teksi aliyekuwa awasaidia kuondoka Mwanza endapo wangefanikiwa kutoroka gerezani.
Kamanda Muliro, alisema mfungwa aliyeuawa ni ni namba 200/2019 George Aloyce (34) ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 15 katika gereza hilo kwa kosa la uhujumu uchumi ambaye alikula njama na kuwashawishi mahabusu wawili ili waweze kutoroka.
Alisema mahabusu wawili ambao pia waliuawa, walikuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji jijini Mwanza ambao kwa pamoja walifanikiwa kutoroka gereza la kuu la Butimba April 14, mwaka huu 12:30 jioni.
“Mfungwa huyu (Aloyce) alifanikiwa kuwashawishi mahabusu namba 3444/2016 Yusufu Benard (34) aliyekuwa na kesi ya mauaji na mahabusu namba 1177/2017, Seleman Seif (28) aliyekuwa akikabiliwa pia na kesi ya mauaji katika moja ya msikiti jijini Mwanza kutoroka kutoka ndani ya ngome ya gereza kuu,”alisema.
Alisema baada ya kuonekana wanakimbia, askari Magereza walipiga filimbi, huku wakiwakimbiza watuhumiwa hao ambapo pia wanananchi wanaoishi jirani na gereza hilo waliitikia na kuanza kuwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu.
“Walipowakamata walianza kuwapa kipigo kikali na baada ya askari Magereza na polisi kufika wananchi waliwakabidhi ili kuondoka nao, lakini hali zao zilikuwa mbaya kutokana na kipigo walichopata kutoka kwa wananchi,”alisema.
Kamanda alieleza polisi kwa kushirikiana na Magereza, waliwachukua na kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure Mwanza ili wapatiwe matibabu, lakini hali ya mahabusu Yusuf Benard na Seleman Seif ilibadilika wakati wakipatiwa matibabu na walifariki dunia.
“Mfungwa George Aloyce alipotibiwa na kuruhusiwa aliomba kwa askari polisi awapeleke eneo la mabatini kwa dereva wa teksi ambaye alidai angewasafirisha kwenda mji mdogo wa Katoro wilayani Geita, baada ya kufanikiwa kutoroka gerezani,”alieleza.
Kamanda alisema walipofika Mabatini akiwa chini ya ulinzi wa polisi akiwa amefungwa pingu, aliomba afunguliwe ili dereva aliyetaka kuwaonyesha asione kama bado kafungwa.
Alisema licha ya askari kukata ombi lake hilo, bado aliifanikiwa kuwakimbia polisi ambao walimkimbiza.
“Mtuhumiwa alipokimbia na askari polisi walimtaka asimame ,huku wakipiga risasi hewani, alikataa kutii amri ndipo polisi wakampiga risasi za miguu na kumkamata lakini walipokuwa wakimpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure alifariki dunia njiani,”alisema.
Kamanda alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na kuwawashukuru wananchi waliojitolea na kushirikiana na askari wanawakamata watuhumiwa hao baada ya kutoroka gerezani.