30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Simbachawene amswekea ndani mkandarasi

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amemsweka ndani Mkandarasi wa Kampuni ya Nangonga Building and Cicil Contractors, Mohammed Nangonga  kutokana na kushindwa kuweka alama za barabarani wakati kampuni yake ikikarabati  mashimo katika barabara ya Dar es Salaam – Morogoro  hivyo kusababisha ajali ambazo zimesababisha  vifo vya watu watatu.

Inadaiwa eneo la Ihumwa ambako ndiko kulikokuwa kukifanyika ukarabati huo juzi kulitokea ajali ambayo iliua watu wawili hapo hapo kutokana na kukwepa shimo. 

Pia jana lori lilokuwa limebeba saruji lilokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kigoma  lilipata ajali ya kugongana na Basi  na hivyo kusababisha kifo cha utingo wa Lori hilo.

Kutokana na ajali hizo,Waziri Simbachawene alifika jana eneo la ajali ambapo alidai Serikali haiwezi kukubali uzembe huo, kwani ajali zimesababishwa na Mkandarasi kutokuweka alama za barabarani wakati akifanya matengenezo.

“Serikali haiwezi kukubali watu wafe tena kwa uzembe hivyo nakuagiza RTO licha ya kwamba huyu ni rafiki yangu mkamate mweke ndani hatuwezi kuwa tunaangalia tu huu uzembe nasema kamata weka ndani pamoja na hawa wafanyakazi wote,”alisema simbachawene.

Mara baada ya kutoa maelekezo hayo Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Dodoma,Nuru Selemani alimkamata Mkandarasi huyo na kumpeleka katika gari la Polisi lilokuwepo eneo hilo.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi,alisema amekuwa akipita katika eneo hilo lakini kumekuwa hakuna alama zozote ambazo zimewekwa kwamba kuna ujenzi unaendelea huku kukiwa na shimo kubwa ambalo limechimbwa.

Alisema Jeshi la Polisi na Wakala wa Barabara (Tanrod) wanatakiwa kutafakari utendaji kazi wao kutokana na uzembe ambao umejitokeza katika neo hilo.

“Nuru (Mkuu wa Usalama Barabarani RTO Mkoa wa Dodoma) hii ni aibu huu ni zaidi ya uzembe mashimo yanachimbwa bila kuwekwa alama yoyote,Tanrod mpo tu mnawaangalia hapa zimetokea zaidi ya ajali nne mnaangalia tu hapana nasema hapana lazima watu wawajibishwe,nimekarika sana,”alisema.

Wakati akiendelea kuzungumza alifika katika eneo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo na kuonesha kusikitishwa kutokana na  kutokuwekwa alama katika eneo hilo.

Mkandarasi aliyekamatwa  Mohammed alisema wamekuwa wakiweka alama lakini wezi wamekuwa wakiiba hivyo kuwapa wakati mgumu wao.

Naye,dereva wa  Lori ambalo limeua mtu mmoja,Shalif Biyibizi raia wa Rwanda  alisema anajisikia vibaya kutokana na kumpoteza Konda ambaye ni rafiki yake,Jean Nsengiyarenye.

Biyinizi alisema ajali hiyo imetokana na yeye  kukwepa shimo lilokuwa katikati ya barabara hivyo kwenda kugongana na basi  hali iliyosababisha Nsengiyarenye kupoteza maisha.

“Naumia sana sana (huku akilia) nimempoteza konda wangu,nilikuwa nimebeba saruji natokea Dar es salaam naelekea Rwanda wakati nakwepa shimo niligongana na basi lilokuwa likienda Dar es salaam lilikuwa likitoka Kigoma.

“Sababu kubwa ya ajali hii ni kutokana na kutokuwa na alama yoyote kuonesha kwamba hapa kuna ukarabati unaendelea na kama unavyoona hili ni shimo kila mtu anajaribu kulikwepa lakini inashindikana,”alisema.

Naye,Shuhuda wa ajali nyingine iliyoua watu wawili,katika eneo hilo,Emmanuel Leonard alisema vijana wawili ambao ni dereva wa bodaboda na abiria wake walifariki juzi kutokana na kukwepa shimo hilo na kwenda kugongana na gari.

“Bodaboda alikuwa akikwepa hili shimo akaenda kukutana na gari wakagongwa wakafa hapo hapo,”alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles