26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mchakato uagizaji treni za umeme waanza

Mwandishi wetu-DODOMA

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, amesema Serikali imeagiza treni tano za kisasa ambazo kila moja itakuwa na mabehewa nane ambayo yatasafirisha abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Pia alisema Serikali haitarudi nyuma wala kusalimu amri, licha ya uwepo wa hujuma zinazofanyika kutaka kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimaendeleo nchini, Dk. Abbas alisema Serikali imeanza zabuni ya kuagiza vichwa 22, vitano vya mafuta yaani dizeli na 17 vya umeme na mabehewa ya abiria 60 na ya mizigo.

“Serikali imeanza zabuni ya treni tano zilizokamilika za abiria zenye mabehewa nane kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar– Moro na kisha Dodoma,” alieleza Dk. Abbasi.

Katika hatua nyingine, alieleza hadi sasa tayari Serikali imeshalipa Sh trilioni 1.07 kutekeleza mradi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere, uliopo Rufiji mkoani Pwani, utakaozalisha zaidi ya megawati 2,000.

“Fedha hizo taslimu Serikali imelipa bila kukopeshwa wala msaada… tayari ujenzi wa sehemu ya kuchepusha maji umekamilika kwa asilimia 100,” alisema.

Aliongeza kuwa wakati wowote wataalamu wataanza ujenzi wa kuta za bwawa hilo.

Pia, Dk. Abbas alisema Serikali inatekeleza ujenzi wa madaraja makubwa katika kuhakikisha huduma ya usafirishaji inaimarika zaidi.

Alisema zimetengwa Sh bilioni 71.4 kwa ujenzi wa daraja la Wami lililopo mkoani Pwani ambalo tayari ujenzi wake umeshaanza.

“Daraja hili kwa kipindi kirefu limekuwa likileta shida hasa kwa magari kupishana. Sasa linajengwa daraja la kisasa ambalo pia barabara zake zitatanulikwa kwa urefu wa kilometa nne kila upande,” alifafanua.

Vilevile alieleza kuwa zaidi ya Sh bilioni 696 zimetengwa kujenga daraja la Kigongo-Busisi ambalo litakuwa refu kuliko madaraja yote ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Dk. Abbas alisema baada ya mkutano wa SADC, Tanzania itaendelea kunufaika na kuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Tamasha la Utamaduni Afrika Mashariki (Jamafest) Septemba 21-28 na litahusisha watu takribani 100,000 kutoka nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan ya Kusini.

“Tamasha hili litafanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Pia, SADC itaendelea kuacha alama muhimu nchini. Mikutano mingine mingi imeanza kuja nchini ukiwemo wa sekta ya habari na mawasiliano katikati mwa Septemba.

“Taasisi zetu zitaendelea kunufaika, mfano MSD imekamilisha mfumo wa kusambaza dawa nchi zote za SADC, TTCL inaendelea kusambaza mkongo wa mawasiliano (Tayari Zambia, Malawi),” alisema.

 Aliongeza kusema kuwa Serikali imejenga madaraja madogo madogo katika wilaya saba nchini kama vile Kondoa (Kisese, urefu mita 38, Sh bilioni 2.08), Kishapu (Manonga, urefu mita 45, Sh bilioni 2.436), Bahi (Chipanga Bridge, urefu mita 45, Sh bilioni 2.11), Iringa (M) (Tagamenda Bridge, urefu mita 30, Sh bilioni 4.5), Songwe (W) (Kikamba Bridge, urefu mita 60, Sh bilioni 1.2), Iramba (Mtoa Bridge, urefu mita 60, gharama Sh bilioni 2.676 ) na Kilombero (Kihansi Bridge, urefu mita 40, Sh milioni 972).

Dk. Abbas alisema Tanzania inaendelea kupiga hatua kwenye mapambano dhidi ya rushwa ikishika nafasi ya kwanza kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mashirika ya kimataifa ya Afro Barometer na Transparency International.

Alisema hadi sasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanikiwa kuokoa Sh bilioni 86, fedha ambazo zilichotwa na mafisadi.

Aidha, alisema Sh bilioni 25 zimerejeshwa serikalini, fedha ambazo zilichotwa kwenye mazingira ya rushwa.

Kwa mujibu wa Dk. Abbas, zaidi ya Sh bilioni 14.6 zimepatikana kutoka kwenye mali ambazo zilipatikana katika mazingira ya kihalifu.

Pia alibainisha kuwa Sh bilioni 10 zimepatikana baada ya kuuzwa mali mbalimbali zilizopatikana kihalifu ikiwemo magari, nyumba na vituo vya mafuta.

Alieleza Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA), imeokoa Sh bilioni 46.9 fedha ambazo malipo yake yalikuwa kinyume na yaliyopo kwenye mkataba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles