23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Ajali yamlaza mtoto kitandani miaka minne

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

NDOTO za mtoto Abdul Mohamed (10) zimefifia baada ya kupata ajali miaka minne iliyopita na kushindwa kuendelea na masomo, huku familia yake na ya dereva wa gari lililomgonga zikivutana.

Baba wa mtoto huyo, Mohamed Hamis, anayeishi  Ulongoni B, Kata ya Gongo la Mboto, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, anadai familia ya aliyemgonga imekataa kumuhudumia mtoto wake na yeye hana uwezo.

Kwa upande wa familia ya dereva aliyemgonga mtoto huyo, inadai ilisimamia matibabu hadi kumfikisha Hospitali ya Taifa Muhimbili na afya yake ikaanza kuimarika, lakini baadaye wazazi wake wakamkatisha matibabu na kuanza kumpa tiba za kienyeji.

ILIVYOKUWA

Imeelezwa kuwa Aprili 3 mwaka 2016 majira ya asubuhi, maeneo ya Ulongoni B, gari lililokuwa likiendeshwa na Kilimo Joseph, lilimgonga mtoto huyo na kumsababishia majeraha mwilini na kushindwa kuendelea na masomo.

Mtoto huyo aliliambia gazeti hili kuwa gari hilo lilimgonga wakati akicheza na wenzake.

“Sisi tulikuwa tunacheza, akachukua gari akaja akanigonga, wakanipeleka hospitali wakanipima kipimo kimoja wakaniacha, nataka kupata matibabu niendelee na kusoma,” alisema Abdul.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Hamis, alisema mtoto wake tangu amepata ajali hakupata huduma kwa familia ya mtu aliyemgonga kwa kipindi chote jambo lililomlazimu kwenda hadi mahakamani ili kuweza kupata haki ya kutibiwa.

“Tumejitahidi mpaka tulipoishia, tumefuatili hiyo kesi lakini hatujui imeishia wapi, tumekwenda mahakamani tunaambiwa tufuatilie hukumu na uwezo wetu ni mdogo, tunaomba Watanzania wenzetu watusaidie,” alisema Hamis.

“Nimekuwa mtu wa kuzungushwa mpaka kesi imeenda mahakamani bila kupewa taarifa, mara ya mwisho kwenda polisi naambiwa kesi ipo mahakamani, nilipofika mahakamani naambiwa nimechelewa kesi imeisha niandike barua ya kumaliza kesi na nipewe karatasi ya hukumu, ndipo nilipomwambia mimi sijui kuandika,” alisema Hamis.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ulongoni, Petro Masalale, alisema mwanafunzi huyo alimsajili mwaka 2016 na kwa bahati mbaya alipata ajali ambayo ilihatarisha taaluma ya mtoto huyo.

Mwalimu Masalale alidai kuwa aliyesababisha ajali hakutoa ushirikiano kwa mtoto huyo.

“Aliyesababisha ajali hajatoa ushirikiano, kwani yeye kama mwanadamu alipaswa kutoa mchango wake wa kumsaidia mtoto huyo jambo ambalo hajalitimiza,” alidai.

Mjumbe msaidizi wa eneo la Ulongoni B, Mtaa wa Mji Mpya, Samson Makanke, alisema mwenye gari lililomgonga mtoto huyo aliitwa na kusema atamuhudumia, lakini akamtelekeza wakati akiwa Hospitali ya Muhimbili.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema wameshangazwa na kitendo cha kinyama anachofanyiwa mtoto huyo kutokana na familia ya aliyemgonga kutomuhudia ili aweze kupona.

Hata hivyo, mmoja wa familia ya aliyemgonga mtoto huyo, Halima Athumani, alikanusha tuhuma hizo na kusema walikuwa wakimuhudumia mtoto huyo ila tatizo mzazi wake alikuja kuchanganya matibabu ya hospitalini na imani za kishirikina.

“Aliyemgonga huyo mtoto ni mvulana ambaye nilikuwa nakaa naye na mtoto alivyogongwa tulikuwa tunajenga, tukahairisha kwanza ili kumuhudumia.

“Tulianza kumuuguza akiwa hospitali ya jeshini baadaye tukaenda Amana hadi Muhimbili tulimuhudumia.

“Baada ya hapo mtoto akawa anaendelea vizuri tu na alikuwa anafanya mazoezi Muhimbili, baadaye wakamwachisha mazoezi wakawa wanasema mtoto wao kalogwa, wakaanza kumpa matibabu ya kijadi ndiyo walivyorudi tena Muhimbili wakaambiwa waanze tena mwanzo,” alisema Halima.

Alidai baada ya mtoto kuendelea kuzidiwa, walimpeleka polisi ambako waliwaambia wazungumzie jambo hilo nyumbani.

“Baada ya kutoka polisi katika mazungumzo mwanzoni tulikubaliana kuwa nitanunua pikipiki ili ifanye biashara mtoto apate matibabu na mahitaji, wakakubali.

“Lakini baadaye wakaja kubadilisha maamuzi, wakaniambia niwanunulie kiwanja halafu niwajengee nyumba, mimi nikawaambia uwezo huo sina,” alidai Halima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles