MBUNGE wa Rorya, Lameck Airo (CCM) amewataka viongozi na wananchi wa kabila la Wajaluo na Wakurya katika Kata za Koryo wilayani Rorya na Bumera wilayani Tarime kutoibiana mifugo.
Amewataka kuzika tofauti zao na kuendeleza ushirikianao, upendo na kuilinda amani iliyopo kwa maendeleo yao.
Kauli hiyo aliitoa alipotembelea kata hizo jirani kwa lengo la kudumisha ujirani mwema baina ya viongozi na wananchi wake.
Alifanya ziara hiyo baada ya mapigano na mauaji ya wananchi makabila hayo yaliyotokea Juni mwaka 2009 wakituhumiana kuibiana mifugo na kusababisha amani kutoweka.
“Viongozi tusimamie na kudumisha amani na upendo lakini pia tuendeleze ushirikiano wetu kwa kuhakikisha tunailinda amani iliyopo.
“Hali hiyo itafanya wananchi wa pande zote mbili waendelee na shughuli za maendeleo ikizingatiwa kuna wakati amani ilipotea na kukatokea machafuko ambako watu walipoteza maisha,”alisema.
Alikuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Bumera (Tarime) mpakani na Kata ya Koryo (Rorya) katika sherehe zilizorejesha ngoma ya asili ya wakurya baada ya kutochezwa kwa kipindi kirefu kutokana na mauaji yaliyofanya ngoma hizo kupigwa marufuku.
“Ombi langu kwa wote wa viongozi wa serikali za vitongoji, vijiji, kata na jimbo tukiwamo wawakilishi wa wananchi tusimamie amani wananchi waendelee na shughuli za maendeleo.
“Tunatambua bila amani hakuna kitu maendeleo, hivyo rai yangu tuilinde amani tukatae wanaochoche na kutuvuruga kwa maslahi yao binafsi na tuwe wajasiri kutoa taarifa kwa viongozi wetu na vyombo vya dola ,”alisema.
Mbunge huyo aliimarisha ujirani mwema kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji baada ya viongozi wa kata hiyo kumweleza hali ya shule za msingi na sekondari kuwa ni mbaya.
Walisema shule hizo zinahitaji kuboresha sakafu kwenye vyumba vya madarasa huku mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Tarime akichangia Sh 500,000 na kumkabidhi Diwani wa Bumera, Marumi kwa ajili ya shule tano.