Na MWANDISHI WETU- DODOMA
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amefanya kikao cha dharura na mameya, naibu meya na viongozi waandamizi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kikao hicho kilifanyika jana mjini hapa katika ofisi za upinzani bungeni ambapo pamoja na mambo mengine, imejadili kuibuka kwa mvutano kati ya Serikali na uongozi wa jiji hilo linaloongozwa na Ukawa kuhusu kuidhinisha Sh bilioni 5.8 za uuzwaji hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa Kampuni ya Simon Group.
Wakati kikao hicho kikifanyika kikao cha Baraza la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Meya, Isaya Mwita, kilichokutana hivi karibuni, kilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kile walichodai ni kubariki vitendo vya kifisadi vya uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi kidogo.
Kikao hicho cha baraza kilikaa kuitikia agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa Januari 27 mwaka huu wakati akizindua mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini humo na kutoa siku tano kwa uongozi wa jiji ili fedha hizo zilizolipwa na Kampuni ya Simon Group, zipangiwe matumizi.
Akizungumzia suala hilo jana nje ya Bunge mjini hapa, Mbowe alisema amewaita mameya na manaibu meya wote wa Ukawa na viongozi waandamizi Ukawa kutoka CUF na Chadema wa Dar es Salaam, ili kuzungumza nao juu ya suala hilo.
“Nimewaita hapa tuzungumze suala hili la Uda ambalo limeibua sintofahamu ya kupata msimamo wa pamoja. Tunahitaji kupata suluhisho la suala hili na hatimaye wakazi wa Dar es Salaam wanufaike na Uda kwa sababu sisi hatuna sababu ya kuiua au kuichukia Uda,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Katika Jiji la Dar es Salaam, Ukawa inaongoza halmashauri tatu ambazo ni ya Jiji inayoongozwa na Isaya Mwita, Ubungo inayoongozwa na Boniface Jacob na Ilala iliyo chini ya Charles Kuyeko.