27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MJANE AMWAGA MACHOZI KWA RAIS MAGUFULI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

MJANE Swabaha Mohammed ameitumia Siku ya Sheria nchini kuwasilisha kilio chake kwa Rais Dk. John Magufuli dhidi ya Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mahakama.

Swabaha aliingia na bango hilo jana na kufikisha kilio chake cha kuporwa haki yake ya mirathi kwa kilio kilichowafanya baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo kuangua vilio.

Mjane huyo alikaa viti vya mwisho katika eneo la watumishi wa mahakama, baada ya Rais Magufuli kumaliza kuhutubia aliinuka huku akimwonesha bango lililoandikwa: Polisi, DPP, Mahakama wanataka kunipora haki zangu’.

Mdai huyo alitoka mahali alikokuwa amesimama na kuanza kwenda mwendo mdogo mdogo kuelekea meza kuu huku wadau mbalimbali wakisikika wakisema nenda mbele.

Kabla ya kufika meza kuu walitokea watu wa usalama na kuanza kumsukuma arudi alipotoka lakini kwa kutumia nguvu huku akiangua kilio aligoma kurudi alipotoka.

Idadi ya waliokuwa wakimzuia mama huyo iliongozekana na kumzidi nguvu hivyo walifanikiwa kumrudisha alipokuwa amekaa japo alifika kwa kuanguka chini kutokana na kuzongwazongwa.

Wakati vurugu hiyo ikiendelea huku mama huyo akilia kwa sauti, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alitangaza kwamba Rais Magufuli amemruhusu mama huyo hivyo aachiwe aende mbele na alipokwenda aliruhusiwa kueleza kisa chake kwa ufupi.

“Wakili kaghushi wosia katika mirathi ya mume wangu kwa kushirikiana na DPP, nina cheti cha ndoa, nilipewa mamlaka na mume wangu, kesi ya mirathi iko Mahakama ya Wilaya ya Tanga lakini hukumu zilitoka mbili, niliyokuwa nayo mimi nyingine na waliyokuwa nayo upande wa pili.

“Nafuatilia haki yangu tangu mwaka 2012, nikienda Polisi naonekana sina maana, nikifika mahakamani sina maana, kila mahali nimefika haki yangu nimenyimwa, nikate rufaa nitapata nini.

“Mama yake marehemu mume wangu yuko hai mahakamani naambiwa amekufa, wanawake wengi wananyanyasika sababu ya haki zao.

“Mimi nadai mali nyingi alizoacha mume wangu, nadhulumiwa na nyingine zinauzwa, natishiwa kuuwawa na nilikutumia sms mheshimiwa Rais ukamuagiza IGP ashughulikie,”alisema.

Swabaha alisema kaamua kufika eneo hilo liwalo na liwe, yuko tayari hata kufungwa lakini apate haki yake.

Kilio cha mama huyo mjane kilifanya wadau wengi waliohudhuria kuangua vilio kwa kumuhurumia alivyoweza kuhangaika tangu mwaka 2012 kutafuta haki yake.

Rais Magufuli alimtaka IGP Ernest Mangu kuelezea tukio hilo baada ya kukubali kwamba analifahamu.

“Mheshimiwa Rais kesi hii ina milolongo mingi , marehemu alikuwa na mke zaidi ya mmoja, mlolongo huo mpaka ulizaa kesi za jinai.

“DCI na DPP wameshughulikia na kuwasaka watuhumiwa, kesi iko mahakamani,”alisema IGP Mangu.

Rais Magufuli aliagiza mama huyo kutafutiwa ulinzi kwa ajili ya usalama wake ili asidhuriwe na ameruhusiwa kuchukua namba ya Jaji Kiongozi, Ferdnand Wambali na kwamba ampigie simu wakati wowote.

Akizungumza na waandishi wa habari alisema mumewe anaitwa Shosi Mohammed, alifariki dunia mwaka 2012 na walifanikiwa kuzaa watoto wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles