UKATA WAKWAMISHA KESI 60 ZA MAUAJI KUSIKILIZWA

0
524

Na Walter Mguluchuma -Katavi

KESI 60 za tuhuma za mauaji zimeshindwa kuanza kusikilizwa mkoani Katavi na Mahakama Kuu ya Sumbawanga kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na mahakama kukosa fedha za kuziendeshea.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi, Chiganga Ntengwa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Mpanda.

Alisema kesi za mauaji ambazo zimeshindwa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya Sumbawanga kwa kipindi chote hicho, zinasababisha kuwapo malalamiko kutoka kwa watuhumiwa.

 Chiganga, alisema ukosefu wa fedha umesababisha mahakama kushindwa kutoa haki kwa wakati kama ambavyo kaulimbiu ya mwaka huu, inavyoeleza kuwa haki itolewe kwa wakati ili kuwezesha ukuaji wa uchumi.

Naye wakili wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Atlles Mlisa, alisema ucheleweshaji wa haki kwa wakati katika mahakama umekuwa ni changamoto ya ukuaji wa kiuchumi kutokana na watu kutumia muda wao mwingi kufuatilia kesi, badala ya kufanya kazi.

Alisema mahakama mbalimbali zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kupata ufumbuzi.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni rasilimali watu, kwamba baadhi ya mahakama kuna tatizo la upungufu wa watumishi, fedha na vitabu vya sheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, aliutaka mhimili huo kutenda kazi kwa kuzingatia haki kwa kila mtu bila kujali kipato.

Alisema mhimili huo hautakiwi kuchelewesha haki bila sababu ya msingi na kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa mengine kwa mujibu wa sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here