25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbinu duni kikwazo maendeleo zao la muhogo

Na JUSTIN DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAKULIMA wa mihogo nchini wamekuwa wakishindwa kunufaika ipasavyo na kilimo cha zao hilo kutokana na kutumia mbinu duni za kilimo na kujikuta wakipoteza nguvu nyingi huku wakiambulia mazao kidogo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya wakulima walionufaika na Mradi wa Kuendeleza zao la Muhogo (ACAI) Wilayani Kisarawe, mkoani Pwani mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Geoffrey Mkamilo, alisema njia pekee ya kuwafanya wakulima kunufaika na kilimo cha muhogo ni kutumia kilimo cha kisasa.

Alisema wakulima wengi nchini wamekuwa wakiamini kuwa kilimo cha muhogo hakihitaji matumizi ya mbolea, jambo ambalo siyo kweli na kuwataka wakulima kutumia mbolea ili waone tofauti.

Dk. Mkamilo alisema mkulima anayetumia mbolea huweza kuongeza mavuno yake kwa asiliami 40 na kuongeza kuwa mihogo inayowekewa mbolea inakuwa na ubora zaidi ukilinganisha na ile ambayo haijawekewa mbolea.

Akitolea mfano katika moja ya shamba la mkulima, alisema: “Shina hili ambalo limeng’olewa kwenye shamba lisilo na mbolea utaona mihogo yake kama ukipima unaweza kupata  kilo moja wakati shina hili ambalo limewekewa mbolea aina mbili yaani Nitrogeni na Potasium uzito wake ni zaidi ya kilo tano,” alisema.

Mmoja wa wakulima aliyenufaika na mradi wa ACAI, Petro Kagusa, alisema mradi huo umeweza kuwaamsha wakulima wengi na kwa sasa wanalima kilimo cha kisasa na hivyo kujihakikishia usalama wa chakula pamoja kuongeza kipato chao.

“Kupitia mradi huu tumeweza kuelekezwa kupanda mbegu bora ambazo hazishambuliwi na magonjwa, kulima kwa kutumia matuta ambayo husaidia muhogo kukua vizuri na pia kurahisisha uvunaji. Mradi huu pia umetufunza umuhimu wa kutumia mbolea na matokeo yake tunapata mazao mengi na bora zaidi,” alisema.

 

Mratibu wa Mawasiliano wa Mawasiliano wa ACAI,  David Ngome, alisema kwa hapa Tanzania mradi huo unatekelezwa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na TARI katika eneo la Kanda ya Ziwa, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini pamoja na Zanzibar, ukilenga kuongeza uzalishaji  na ubora wa zao la muhogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles