30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NEMC yakifungia kiwanda cha nyama ya punda

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

BARAZA la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), limekifungia kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilichopo kwenye Jiji la Dodoma, baada ya ukaidi wa muda mrefu wa mmiliki kufuata taratibu sahihi za uhifadhi wa mazingira.

Barua iliyoandikwa na Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Vedast Makota,  imeeleza kwamba, kiwanda hicho ambacho kinashughulika na uchinjaji na usafirishaji wa nyama ya punda nje ya nchi, kwa muda mrefu sasa kimeonyesha kushindwa kuzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira, licha ya onyo na ukumbusho kadhaa uliofanywa na baraza.

“Kufuatia mlolongo huu wa uchafuzi wa mazingira, ambao umekuwa ni kero kwa majirani na ambao unaleta mashaka kwenye ubora wa bidhaa, Baraza limefikia hatua ambayo linakosa cha kushauri zaidi ya kufunga kiwanda,” imeeleza barua hiyo.

Kwenye maelezo ya ufungaji wa kiwanda hicho, Dk. Makota alisema: “Kwa mamlaka yaliyokabidhiwa kwa Baraza chini ya Kifungu cha 196(2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, unaamuriwa kusimamisha shughuli zote za uzalishaji kuanzia siku ya agizo hili mpaka utakapochukua hatua kikamilifu za kutekeleza maagizo yote uliyopewa hapo awali,” ilieleza barua hiyo

Kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na kampuni inayofahamika kama Huwachen Company Limited, kimekuwa kwenye mvutano wa muda mrefu na Baraza pamoja na Wizara inayohusika na uhifadhi wa mazingira tangu Mei, mwaka huu, ambapo aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, alitembelea na kueleza kutoridhishwa kwake na hali ya uhifadhi wa mazingira.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri ilitokana na ukaguzi wa NEMC uliofanywa Agosti, mwaka huu kwa lengo la kutathmini hali ya uhifadhi wa mazingira kwenye kiwanda hicho kutokana na shughuli zake. Katika tathmini hiyo, suala la uchafuzi wa mazingira liliendelea kuonekana kuwepo.

Mambo yaliyoonekana kuwa ni tatizo ni pamoja na mabaki ya damu kwenye eneo hilo ambayo yalipelekea uwepo wa nzi wengi, kuziba kwa mitaro ya kupitisha maji machafu, kukosekana kwa utaratibu madhubuti wa kuhifadhi mbolea, kiwango duni cha shimo la kuhifadhia uchafu, harufu mbaya na ukosekanaji wa mpango endelevu.

Mapungufu hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa NEMC yanakiuka vifungu kadhaa vya sheria ya mazingira ya mwaka 2004, hii ni pamoja na kifungu cha 106 (1) (2) na (6) pamoja na kifungu cha 187 (1) (b) na (C).

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles