NA AZIZA MASOUD,
MAZOEZI hujenga afya ya binadamu  na kuweka viungo katika hali ya ukakamavu.
Kuna aina mbalimbali za mazoezi kulingana na umri, uzito na madhumuni ya kufanya hivyo.
Kwa watoto mazoezi huwasaidia kunyoosha viungo, kumfanya awe na viungo shupavu pamoja na kuondoa woga.
Mazoezi ya watoto wadogo yanatofautiana na wanayofanya wakubwa, watoto wanapaswa kufanya mazoezi madogomadogo.
Ni muhimu walezi au wazazi kuweka ratiba maalumu ya kumfanyisha mtoto mazoezi.
Kwa watoto wa umri kati ya siku 30 mpaka miezi sita, anakuwa na viungo laini hivyo mazoezi yake hayahitaji kutumia nguvu kubwa.
Mazoezi ya watoto hawa  mara nyingi hushauriwa yafanyike asubuhi na jioni, utaratibu ambao unapaswa kuwekwa na mzazi.
Baadhi ya wazazi hupenda kuwafanyisha watoto mazoezi  baada ya kumaliza kuoga wakati wa asubuhi na jioni.
Unapomaliza kumuogesha mtoto unaweza kuanza kumrusha rusha juu taratibu huku ukimuimbia nyimbo.
Zoezi la kumrusha unapaswa ulifanye si chini ya mara tano, kwa siku za mwanzo mtoto atakuwa analia kwa woga usiogope endelea kumrusha mpaka atakapozoea.
Mbali na kumrusha, yapo mazoezi ya kumnyoosha miguu  na mikono bila kutumia nguvu.
Unapaswa ushike viungo hivyo na kumnyoosha miguu kidogo kidogo na mikono kwa kuikunja kwa uangalifu bila kutumia nguvu.
Fanya zoezi hilo taratibu bila kumsababishia mtoto maumivu, huku ukimuimbia nyombo za hapa na pale.
Pia unaweza kunyoosha viungo kwa kutumia mafuta ya nazi kwa mtindo wa masaji ambayo inasaidia kunyoosha viungo.
Mafuta unayotumia unaweza kuanza kuyaweka kwenye moto kidogo na kuyatoa kabla hayajapata joto sana.
Mnyooshe taratibu kwa uangalifu kiungo kimoja kimoja angalia usimuumize.
Masaji hufanywa taratibu kwa kutumia viganja vya mikono, mnyooshe  mtoto mgongo, miguu na vidole kwa mafuta ya nazi, ama mafuta laini yaliyotengenezwa kwa ajili ya watoto.
Mtoto hapaswi kufanya mazoezi kama atakuwa ametoka kula chakula, anaweza akatapika wakati ukiendelea na mazoezi.
Baada ya kumfanyisha mazoezi, muandae mtoto wako vizuri kwa kumvalisha nguo na kumuacha apumue.