24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TUMWACHE RAIS AFANYE YAKE

KABLA ya Rais Dk. John Magufuli
KABLA ya Rais Dk. John Magufuli

Na JOHN MADUHU-MWANZA

KABLA ya Rais Dk. John Magufuli, hajaanza ziara ya siku tatu ya kikazi mkoani Kagera, kulikuwa na taarifa mbalimbali zilizokuwa zikichapishwa katika mitandao ya kijamii pamoja na magazeti, zikihoji kwanini hajaenda kuwatembelea waathirika wa tetemeko lililotokea Oktoba mwaka jana mkoani humo.

Wanasiasa wachovu waliopiga kelele na porojo za kwanini Rais hajaenda Kagera zimezimwa rasmi baada ya mkuu huyo wa nchi kufanya ziara na kuwapa pole wananchi waliokumbwa na tetemeko.

Katika ziara hiyo, Rais alitembelea maeneo mbalimbali yaliyokuwa yameathiriwa na kuzungumza na wananchi.

Rais Magufuli alitoa msisitizo kuwa Serikali yake kamwe haitaweza kuwajengea nyumba wananchi badala yake wananchi hao wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujenga nyumba zao zilizobomolewa.

Alisema Serikali yake itahakikisha inarejesha miundombinu ya barabara, shule, hospitali, vituo vya afya ili viweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

Kama kawaida ya wanasiasa ambao hapo awali nimewaita wachovu, wamedandia na kuanza kupotosha kauli ya Rais Magufuli kuhusu kile alichokisema mkoani Kagera.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo vya habari, wanasiasa hao wamekuwa wakilaani kauli iliyotolewa na Mkuu wa nchi kuhusu msimamo wa Serikali kutowajengea nyumba wananchi ambao nyumba zao ziliathiriwa na tetemeko hilo.

Siku zote Rais Magufuli amekuwa akisema wazi kuwa ‘msema ukweli ni mpenzi wa Mungu’, Rais asingeliweza kubadili kauli yake ambayo aliitoa hapo awali wakati akipokea misaada mbalimbali ya kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera.

Rais alitoa msimamo wa Serikali kuwa kamwe fedha na misaada mbalimbali inayotolewa atahakikisha inawafikia walengwa na kuonya kuwa wale ambao watabainika kujinufaisha na misaada hiyo watachukuliwa hatua kali.

Ndio maana tuliona hatua alizochukua Rais kwa kuamua kutengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kagera, kutokana na kubainika kufungua akaunti ya maafa kinyume na utaratibu.

Pia, alisisitiza kuwa kamwe Serikali yake haitajenga nyumba kwa wananchi, badala yake itatoa mchango kidogo kwa ajili ya wananchi hao ambapo tayari baadhi ya wananchi wamekabidhiwa mabati pamoja na mifuko ya saruji.

Dk. Magufuli si aina ya wanasiasa vigeugeu wanaobadilika kulingana na mazingira ili kuwafurahisha wananchi au wapiga kura, siku zote kiongozi huyo amejipambanua kuwa ni kiongozi anayefuata haki, sheria na taratibu katika utendaji wake wa kazi.

Kauli ya kutowajengea nyumba wananchi ambao wamepatwa na maafa pia amewahi kuitoa mkoani Shinyanga, baada ya wananchi wa Kijiji cha Mwakata nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua.

Gumzo la Rock City linawaomba Watanzania tumuunge mkono Rais Magufuli katika harakati zake za kuijenga nchi badala ya kutumia siasa kumbomoa, kama ambavyo inafanyika hivi sasa.

Kwa mtu mwenye akili timamu na mwenye mapenzi mema na nchi yake, inaingia akilini kweli unaamua kumpinga Rais kutokana na kauli yake ya kutaka fedha zisitumike kujenga nyumba za watu binafsi na badala yake zitumike kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko.

Miundombinu hiyo imekuwa ikitumiwa na wananchi wote bila kujali itikadi ya siasa, miundombinu hiyo imejengwa na Serikali kwa gharama kubwa pasipo kujali itatumiwa na wananchi wa vyama gani.

Leo hii Watanzania wamejawa na ubinafsi, wametanguliza vyama na itikadi za kisiasa wanapojadili masuala ya nchi, uzalendo umetoweka.

Ni ukweli usiopingika kuwa Rais au Serikali yake hawakupanga tetemeko hilo la ardhi litokee mkoani Kagera, kwa maana halisi ni kuwa Serikali haikuwa na bajeti maalumu ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na tetemeko hilo.

Kiasi kidogo kilichokuwepo pamoja na misaada ya nchi rafiki na Watanzania wenye uwezo, ndicho hicho kilichotolewa kuwasaidia ndugu zetu, hao wanaopiga kelele hadi leo hii wameshindwa kurejea mkoani Kagera kuwasaidia wananchi hao.

Kama kawaida yao walionekana siku za awali na kupigwa picha na kuonekana katika vyombo vya habari, ndiyo ikawa mwanzo na mwisho wao, wakaamua kukaa pembeni kuchungulia nani amekwenda mkoani Kagera na nani hajaenda ili watoe shutuma.

Wamefanikiwa kumwona rais amekwenda Kagera, walikuwa wakivizia atazungumza nini ili waonekane tena katika vyombo vya habari kumpinga kwa kile atakachozungumza baada ya kukutana na wananchi.

Gumzo la Rock City lina imani na Serikali ya Rais Magufuli kwa namna ambavyo ameonyesha utumishi uliotukuka katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Tanzania ya leo ni mojawapo ya nchi ambazo zimefanikiwa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake kwa kiwango cha juu, Serikali imefanikiwa kudhibiti rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na uzembe uliokuwepo.

Rais nafahamu unajua kuwa umekuwa ukipigwa vita ndani ya CCM na nje ya CCM, najua unafahamu kuwa siku zote wapinzani kamwe hawawezi kukusifia kwa kazi unazozifanya, kitu muhimu na cha msingi ni kuwa Watanzania tunakuelewa kwa kile unachokifanya na tuko nyuma yako na tunakuunga mkono hivyo usikate tamaa.

Kundi la watu linalokupiga vita ni lile ambalo ndugu na jamaa zao wamekutana na pangua pangua yako maarufu kama kutumbua majipu, uliyafanya hayo si kwa ajili ya kumuonea mtu yeyote bali ulichukua hatua ili kuhakikisha Tanzania haiendelei kuwa shamba la bibi.

Tumwache Rais wetu atekeleze majukumu yake, Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.

Naomba kuwasilisha.

[email protected]

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles