NA PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
UPANDE wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaachia huru watu 31 wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kesi ya kufanya mikusanyiko isiyo halali.
Hoja hiyo ilitolewa jana baada ya Wakili wa Jamhuri, Faraji Nguka, kudai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile kuwa kesi hiyo ilikuwa kwa ajili ya kusomewa kwa maelezo ya awali (PH) kwa washtakiwa, lakini wameshindwa kuandaa jalada kwa madai kuwa lipo polisi.
Wakili Nguka alidai washtakiwa 15 hawajafika mahakamani, hivyo basi walishatoa hati ya kukamatwa na kuiomba mahakamani hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Alex Masaba alidai kwa mujibu wa sheria, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wanapotekeleza majukumu yao ikiwamo ya kuwashtaki, wanatakiwa kutenda haki kwa washtakiwa na kulinda haki zao.
Alidai kwa mwenendo wa wakili wa Jamhuri tangu kesi imefunguliwa Februari mwaka 2018, mpaka sasa imefika miezi 13 ni dalili kwamba haki ya washtakiwa imekiukwa.
Wakili Masaba alidai mpaka sasa taratibu za mahakama zimekiukwa kwa mujibu wa kifungu cha 225(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai ambayo inaelezaa kesi inapofunguliwa inatakiwa ianze kusikilizwa kwa miezi sita lakini mpaka leo imefika miezi 13.
“Ninaomba mahakamani yako kuwaachia huru washtakiwa hawa kwa sababu upande wa jJamhuri umekiuka taratibu za uendeshaji wa kesi,” alidai wakili Masaba.
Hata hivyo, wakili Rwizile aliutaka upande wa Jamhuri kuchagua kuendelea na kesi hiyo bila ya kuwapo washtakiwa hao kesi hiyo itakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na PH.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 22, 2018 katika kesi ya jinai namba 51/2018 na kusomewa shtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa hao ni pamoja na Thabita Mkude, Haji Lukwambe, Emmanuel Kimoi, Mohammed Juma, Hussein Mrombo, Abdallah Hamis, Hussein Kidda, Paulo Kimoro, Brayan Morris, Hussein Nguli na Edna Kimoro.
Wengine ni Jonathan Lema, Salha Ngondo, Ramadhan Mombo, Godwin Mwakasungura, Hassan Kibweda, Omary Hamad, Fatima Ramadhan, Ezekiel Nyenyembe, Denis Mtegwa, Dickson Kerefu, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa, Mussa Kusigila.
Wengine ni Omary Danga, Jackson Masilingi, Asha Kileta, Ally Rajabu, Isack Ng’aga, Erick John na Aida Olomi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa Februari 16, mwaka 2018 huko Kinondoni Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali.