32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

MATUMIZI MASHINE EFD MUHIMU KATIKA UFANISI WA KODI

Na KOKU DAVID

KATIKA kuhakikisha usalama wa kodi inayotolewa na walipakodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuwasisitizia wafanyabiashara kutumia mashine za kodi za Kielektroni (EFDs).

Kwa kutumia mashine za EFD, kodi stahiki itafika serikalini na pia mteja atakuwa na uhakika kuwa kodi aliyolipa imefika sehemu husika.

Kama ambavyo TRA imekwishatolea elimu kuwa mashine za EFD, zinamsaidia mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zake kwa zaidi ya miaka mitatu.

Sambamba na wafanyabiashara pia mashine hizo zinaisaidia Serikali kupata kodi zake stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mashine hizi ambazo hivi sasa zimeboreshwa ili kuhakikisha wafanyabiashara ambao si wazalendo hawazichezei kwa mara ya kwanza, zilianza kutumika mwaka 2010.

Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianzisha mfumo wa matumizi ya mashine EFD ili kumrahisishia mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zake.

Pia mfumo huo ulilenga kuondoa changamoto wakati wa ukadiriaji wa kodi pamoja na kuweka uwazi kwa mfanyabiashara ambao utamwezesha kujua kodi anayotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria.

Matumizi ya mfumo huo yalianza kutumika kwa awamu mbili na kwamba katika awamu ya kwanza ilianza kutumiwa na wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Awamu ya pili ya matumizi ya mfumo huo ilihusisha wafanyabiashara ambao hawakusajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani VAT ambao mauzo ghafi yao kwa mwaka ni zaidi ya Sh milioni 14.

Sambamba na kuwasaidia wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao, pia matumizi ya mfumo huo yamesaidia kutopotea kwa mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa TRA, sheria ya kusimamia awamu ya pili ya mfumo wa mashine za EFDs ni ya kanuni ya kodi ya Mapato (Income Tax Electronic Fiscal Devices Regulations, 2012).

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema kutokana na mfumo huo, mfanyabiashara au mwananchi anapolipa kodi inaisaidia Serikali kufanya maendeleo katika mambo mbalimbali.

Anasema utaratibu wa mfanyabiashara kutoa risiti kwa mteja baada ya kumhudumia anakuwa amemhakikishia kuwa kodi aliyolipa kutokana na bidhaa aliyonunua imefika sehemu husika.

Anasema sheria inamtaka kila mfanyabiashara anayefanya mauzo au kutoa huduma kwa mteja wake inayoanzia Sh 5000  na kuendelea anatakiwa kutoa risiti.

Anaongeza kuwa TRA imeweka mikakati kuhakikisha inawaondolea changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kulipa kodi pamoja na kufanya biashara kwa uhuru.

Kayombo anasema kwa upande wa mamlaka hiyo, changamoto inayokutana nayo ni baadhi ya wafanyabiashara kukosa uaminifu kutokana na kutozitumia mashine za EFD kama ambavyo sheria inavyotaka na kuongoza.

Anasema pia baadhi ya wafanyabiashara hutoa risiti feki yaani zenye bei pungufu tofauti na huduma walizotoa au risiti zisizotambuliwa na mamlaka, huku wengine wakiacha kutoa kabisa risiti baada ya kutoa huduma. Mambo yote mawili ni makosa ya jinai.

Anasema wafanyabiashara pamoja na walipakodi wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanatoa risiti baada ya kutoa huduma na walipakodi wanatakiwa kukumbuka kudai risiti baada ya kuhudumiwa kwani ni haki yao stahiki.

Anasema ili kuhakikisha sheria ya matumizi ya mashine za EFD inatekelezwa, TRA inaendesha zoezi endelevu la usimamizi wa kuhakikisha EFD zinatumika kikamilifu na kwamba kila mfanyabiashara anatakiwa kutii sheria ili kuepuka usumbufu wa kufikishwa mbele ya sheria.

Anasema kwa wafanyabiashara ambao si rasmi, wanatakiwa kurasimisha biashara zao ili waweze kuingia katika wigo wa kulipa kodi na kutumia mashine za EFD. Ni heshima kubwa kuwemo kwenye orodha adhimu ya walipa kodi wa nchi.

Kayombo anasema ili kurahisisha upatikanaji wa EFD, wasambazaji wa mashine hizo walisogeza maduka  yao Kariakoo na kwamba baada ya kuwauzia pia wanawapa elimu ya namna ya kuzitumia na mpangilio wa huduma baada ya mauzo.

Anasema kwani wasambazaji hao wanawajibika kuzitengeneza mashine hizo iwapo zitaharibika kwa bahati mbaya au katika muda wa udhamini (warranty).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles