Na Mwandishi Wetu, Arusha
MASHIRIKA matatu yasiyo ya kiserikali wamezindua mradi wa kuwajengea uwezo,uelewa na ujasiri wanawake vijana ili watumie mitandao ya kijamii, katika kudai haki za kijamii,kisiasa na kiuchumi.
Mashirika hayo ni Shirika la Waandishi wa Habari la Utetezi wa Jamii za Pembezoni(MAIPAC),Shirika la Ustawi wa Wanawake na Watoto(WOCWELS) na Taasisi ya Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO).
Akizungumza jana jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mradi huo utakaogharimu sh milioni 9, Mwakilishi wa Shirika la MAIPAC, Musa Juma amesema wamezindua mradi huo wa mitandao ya kijamii kwa lengo la kuendeleza wanawake wa vyuo vikuu kielimu na kuwaunganisha pamoja ili wapambane na suala la ukatili.
Amesema mradi huo wa miezi mitatu utanufaisha wanafunzi 90 kutoka vyuo vikuu vya Tumaini Makumira, St.Augustine tawi la Arusha na Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Amesema wanaamini kupitia mradi huo utawasaidia wanufaika kutangaza biashara zao na kujiinua kiuchumi.
Juma ameeleza kuwa wanataka matumizi makubwa ya Tehama kwa wanafunzi kwa sababu wanafahamu wanawake wanakabiliwa na changamoto katika jamii, hivyo wameona kupitia mitandao ya kijamii wanaweza wakawaunganisha wanafunzi wanawake vijana waliopo katika elimu ya juu kujiendeleza.
“Badala ya kutumia hii mitandao kwa vitu ambavyo sio vya maana sana watumie kujiendeleza kielimu, tumeona kuwa hii ni njia rahisi ya siku hizi ya kuwafikia watu wengi na kutoa elimu ili weweze kutumia kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa kijinsia,”amesema.
Naye Odero Odero kutoka CILAO amesema katika kipindi cha utekelezaji wa mradi watatoa mafunzo kwa wanufaika hao juu ya usalama katika mitandao na sheria na sera zinazotumika kulinda mtandao ndani na nje ya nchi.
“Lakini tutaendesha mdahalo kuhusu matumizi ya mitandao na kueleza fursa na changamoto zilizopo,”amesema.
Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la WOCWELS, Mary Mushi, amesema wameamua kuwajengea ujasiri watoto wa kike kupitia mitandao ya kijamii na kuwaomba wasiogope pale wanapokutana na vitendo vya ukatili, watoe taarifa na kujitokeza kupinga matukio hayo.
“Tunataka tujenge ujasiri kwa watoto wa kike lakini pia na wao wajione ni sehemu ya kuleta mabadiliko kwa jamii kupitia mitandao ambapo tunatoa mafunzo kwa wasichana 30 kutoka vyuo vitatu ambao hawa ndio watakuwa mabalozi wa kufikisha elimu hii kwa jamii,”amesema Mushi.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Ester Koka kutoka Chuo Cha Tumaini amesema kuwa mradi huo utawasaidia kupata nafasi ya kutoa ya moyoni kuhusiana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wanawake vijana ikiwamo udhalilishaji kwa kuweza kupaza sauti zao kupitia mitandao.