UIGE, ANGOLA
MASHABIKI 17 wa soka nchini Angola, wameripotiwa kufariki dunia baada ya vurugu zilizotokea juzi nchini humo wakati wa mchezo kati ya Recreativo do Libolo dhidi ya Santa Rita de Cassia.
Vurugu hizo zilisababishwa na baadhi ya mashabiki kuingia uwanjani kwa nguvu kushuhudia mchezo huo kwenye mji wa Uige, uliopo Kaskazini mwa Angola.
Imeripotiwa kuwa mashabiki wengine 60 wamejeruhiwa vibaya baada ya vurugu hizo ambapo watu wengi walikanyagana. Baada ya muda taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na picha mbalimbali za tukio hilo.
Msemaji wa hospitali nchini humo ambako majeruhi wanapatiwa matibabu, amesema vifo vya wengi vilisababishwa na kukanyagana huku wengi wao wakikosa hewa ya kutosha. Tayari Rais wa nchi hiyo, Jose do Santos, ameamrisha uchunguzi kufanyika.
Mchezo huo ulikuwa wa kwanza msimu huu katika michuano ya Ligi Kuu nchini humo, huku ikionekana kuwa na msisimko wa hali ya juu.