25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

JPM AKOLEZA MOTO DAWA ZA KULEVYA

Na NORA DAMIAN

RAIS  Dk. John Magufuli amezidi kukoleza moto wa mapambano ya vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.

Ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika mapambano hayo kwa kuhakikisha vinasimamia sheria ipasavyo   kukabiliana na tatizo hilo.

Vilevile,  amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara  hiyo haramu ya dawa za kulevya.

Rais amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na wanaotumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa.

Alitoa kauli hiyo   Ikulu,  Dar es Salaam jana, alipomwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga, Kamishina wa Uhamiaji Dk. Ana Makakala na mabalozi watatu walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Hao ni Balozi wa Algeria, Omar Yusuph Mzee, Balozi wa Ubelgiji, Jospeh Sokoine na Balozi wa Uganda, Grace Mgovano.

 

Alisema vita ya dawa za kulevya haiwezi kwenda kwa mzaha ni lazima wakuu wa vyombo vya dola wahakikishe wanasimamia sheria namba 5 mwaka 2015.

Rais  alimtaka Kamishna Siyanga kufanya kazi kwa nguvu zote bila kuangalia sura, rangi ama cheo cha mtu.

Alisema Sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kupambana na dawa za kulevya inaipa   Serikali mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya na kwamba wanaoona haifai waende bungeni wakaifanyie marekebisho.

 “Hii ni vita kubwa, hakuna Mtanzania yeyote anayelipenda taifa lake akalichukulia suala hili kwa mzaha.

“Tukilipeleka kwa mzaha tutaangamia na tutakwenda kujibu kwa Mungu kwa nini tulinyamaza, adhabu ipo mikononi mwetu,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Rais  alitafsiri maana ya Serikali kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na mtu yeyote atakayepewa mamlaka ya kusimamia serikali.

“Sheria imetupa mamlaka hayo na kifungu namba 10 kimeeleza wazi, lakini kama kuna watu wanafikiri hiyo sheria  haifai waende wakaifanyie amendment (mabadiliko) bungeni watoe hicho kifungu.

“Najua tumeelewana na wanaonisikia wamenielewa. Hatutajali mbunge, waziri, mwanasiasa, mchungaji, padri, sheikh, mkubwa au mtoto tutadili naye,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Alimtaka Kamishna Siyanga kufanya kazi kwa nguvu zake zote na kusimamia sheria bila kumwonea mtu.

“Nimeambiwa wewe ni mmasai na ninavyojua wamasai huwa hawaogopi… kama wanaua simba hutaogopa dawa za kulevya, serikali iko pamoja na wewe na Mungu yuko pamoja nawe lazima tuokoe roho za Watanzania hasa vijana wetu,” alisema.

Mabalozi na dawa za kulevya

Pia aliwataka mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania nje kutowatetea Watanzania watakaokamatwa au kutiwa hatiani kutokana na makosa ya dawa za kulevya na badala yake wafanye kazi ya kuijenga Tanzania katika uchumi.

“Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi wote msijihusishe na Watanzania waliofungwa nje kutokana na dawa za kulevya, waacheni wapate chakula wanachostahili.

“Kama ameshikwa kwenye nchi ambayo sheria zake ni kunyongwa mwache anyongwe huko huko.

“Nalisema hili kwa dhati na wala simung’unyi maneno, tukichekacheka Taifa letu litapoteza nguv kazi kubwa,” alisema.

Rais Dk. Magufuli alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na viongozi wote walioanza kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.

“Tatizo hili linaliangamiza Taifa, wako vijana wengi katika taifa letu wana mikono na miguu lakini hawawezi kufanya chochote kwa sababu ya dawa za kulevya na wengine wamepoteza maisha.

“Ukishikwa na dawa za kulevya hata kama wewe ni kiongozi wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) haina maana kwamba CCM inahusika, kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe,” alisema.

UTEUZI KAMISHNA DAWA ZA KULEVYA

Rais Magufuli alisema licha ya sheria kupitishwa na kusainiwa hakuwahi kufikishiwa  mapendekezo ya kuunda mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya.

“Hata Waziri Mkuu hakujua kama yeye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kupambana na Dawa za Kulevya, kama kujua amejua jana au juzi.

“Sina uhakika kama mawaziri ambao mmetajwa na sheria hii kama wajumbe mlikuwa mnajua. Mlifichwa na wale wanaosimamia.

“Hata mimi sikuletewa mapendekezo ya kumteua kamishina hadi nilipoamua juzi kumteua mwenyewe kutokana na vyanzo vyangu vingine. Hivyo mnaweza kujua ni kwa namna gani vita hii ilivyo kubwa.

“Sheria isingekuwa imekutaja wewe (Waziri Mkuu) ningejipa mimi mwenywe uenyekiti wa baraza hili, lakini sitaki kuvunja sheria. Na ninyi mawaziri simamieni sheria mmekuwa waogawaoga hivi…Mungu ndiye amewapa hii nafasi,” alisema.

Kuhusu Kamishina wa Uhamiaji, alisema idara hiyo imekuwa na changamoto kubwa hasa katika kitengo cha fedha.

Alimwagiza kamishna huyo kwenda kuifumua na kuisuka upya.

Alisema yamekuwapo matatizo ya hati hewa za kusafiria, watu wasiostahili kupewa uraia na wasiostahili kupewa hati za kusafiria za hadhi ya diplomasia.

“Mfano mzuri tu mwaka jana tulipata ugeni mkubwa wa ndugu zetu mabohora walioamua kuja kufanya sherehe zao hapa nchini.

“Washiriki walikuwa 32,000 ukipiga hesabu tulitegemea tungepata fedha za kutosha. Lakini niliuliza fedha zilizopatikana ni kiasi gani hadi leo sijapata jibu na taarifa nilizopata ni kwamba wengi hawakulipa fedha.

“Nimechagua mwanamama kwa sababu kina mama ni waaminifu kwa hiyo kufeli kwako ni kufeli kwa kina mama wote, usiogope sura tunataka uende ukafanye mabadiliko,’ alisema.

APONGEZA BUNGE LA 10

Katika mkutano huo, Rais Dk. Magufuli alitumia muda mwingi kumpongeza Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anne Makinda, kwamba lilikuwa la uzalendo. 

“Baada ya kuona sheria ilikuwa haina nguvu wabunge wa wakati ule walisimama pamoja bila kujali vyama vyao wakapitisha sheria hii.

“Nampongeza sana Rais Kikwete hakuchelewa akaisaini kwa sababu alijua madhara ya dawa za kulevya katika nchi yetu.

“Wako wengine wamejitokeza wamesema wameingiliwa mamlaka yao wakati na wao wameingilia mamlaka ya kuwaita wengine.

“Waziri Mkuu usiogope chochote kasimamie sheria, hata kama wakikupigia kura ya kutokuwa na imani usiogope hukuzaliwa kuwa Waziri Mkuu,”alisema Rais Dk. Magufuli.

VYOMBO VYA ULINZI

 Rais Magufuli pia alionyesha kukerwa na tabia ya baadhi ya watu wasioheshimu vyombo vya ulinzi na usalama na kuyataka majeshi yote kusimamia mapambano hayo.

“Vyombo vyetu saa nyingine vimekuwa jipu. I wish ningekuwa IGP (Natamani ningekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi), yaani mtu anakwenda kuripoti polisi halafu anakwenda kupiga deki gari lake kwani mliambiwa pale mnasafisha magari na polisi mpo tu…mtu anakwenda kuimba polisi.

“Kamishna Sirro (Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam), akaitika na kusimama. Ulitaka kuimbiwa   mapambio (hapana mkuu) sasa sitaki kusikia tena wakija kuimba shika wote wakaimbie lock up (mahabusu).

“Tumefika mahali watu tumekuwa na dharau, mambo ya msingi tunayapeleka kimzaha, mbona hawajaenda Lugalo kuimba mapambio.

“CDF (Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama) wangekuja kukuimbia mapambio kweli pale Lugalo..sasa nataka vyombo vya ulinzi viheshimike, mko pale kwa ajili ya kutekeleza sheria tukileta mzaha katika masuala haya tutakuja kujuta sisi wenyewe,” alisema.

WATANZANIA WALIOFUNGWA NJE

Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alieleza  kuwa Watanzania zaidi ya 500 wamefungwa nje kutokana na dawa za kulevya.

Lakini Rais Dk. Magufuli alisema takwimu alizonazo ni zaidi ya 1,000 na kwamba 68 kati yao wamehukumiwa kunyongwa nchini China.

Takwimu zilizotolewa na Waziri Mkuu zinaonyesha zaidi ya Watanzania 200 wamefungwa   China, Afrika Kusini (296), Ethiopia (7), Iran (63) na Brazil (12).

Pia alisema kwa mwaka jana dawa za kulevya zilizokamatwa ni bangi (kilo 3,798.5) huku kesi zilizoko mahakamani zikiwa 934, mirungi (kilo 1,814) na kesi zilizoko mahakamani ni 135, heroin (kilo 50.5) kesi zilizoko mahakamani ni 292, cocaine (kilo 5.4) na kesi zilizoko mahakamani ni nne.

Takwimu zilizotolewa na Rais Dk. Magufuli zinaonyesha Watanzania waliofungwa Msumbiji ni (20), Nepal (4), Iran (63), India (26), China (265), Uturuki (38), Ugiriki (25), Afrika Kusini (296), Brazil (100 – 120), Malaysia na Thailand (16), Indonesia (1), Comoro (3), Pakistan (15), Japan (6), Nigeria (1), Ghana (1), Uingereza (22), Kenya (66), Misri (2) na Uganda (15).

Alisema licha ya kesi zilizotajwa, kwa Dar es Salaam pekee katika Mahakama Kuu kuna kesi zaidi ya 50.

Rais alivitaka vyombo vyote vinavyohusika kutoa ushahidi   kesi hizo ziweze kusikilizwa haraka na kutolewa hukumu.

Pia aliziomba jumuiya ya kimataifa kusaidia katika vita hiyo   kuokoa Watanzania hasa vijana wasiangamie.

“Vita hii ni kubwa hata kama hatutaweza kushinda kwa asilimia 100 lakini tunataka tuipunguze kwa manufaa ya vijana wetu,” alisema.

BOSI DAWA ZA KULEVYA

Akizungumza na MTANZANIA baada ya kuapishwa, Kamishna Sianga alisema mkakati wa kutangaza majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya utaendelea lakini utafanywa uchunguzi kwanza.

“Huu ni mkakati ambao umeanzishwa na serikali kwamba hatutaficha majina ya watu lakini tutafanya uchunguzi wa hao watu kama kweli wanajihusisha na dawa za kulevya ndipo tuchukue hatua,” alisema.

Pia alisema unaangaliwa uwezekano wa kuhamishia hatua ya  kuwahoji watu wanaotumia au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika mamlaka hiyo.

“Huko nyuma hili jambo lilikuwa linashughulikiwa na vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria peke yake lakini hivi sasa linashirikisha wadau wengi ambao ni watu muhimu katika vita hii.

“Tutaangalia njia kuu za usafirishaji dawa za kulevya, kuna ‘Southern route’ ambayo inatoka Pakistan na Iran inakuja hadi Pwani ya Uajemi halafu dawa zinakuja nyingi kwenye majahazi.

“Tutapambana nao kwenye maji. Kwa hawa wanaolima tutapambana na bangi na mirungi kwa sababu haya madawa ndiyo yanawaumiza Watanzania kuliko heroine na cocaine, tutahakikisha tunaondoa katika mikoa ile wanayolima halafu tutaendelea kupambana na dawa nyingine,” alisema.

Alisema kuna mkakati wa kutoa elimu kwenye vyuo na taasisi zote   watu wasijihusishe na dawa za kulevya.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na makatibu na mawaziri mbalimbali ambao waliagizwa na Waziri Mkuu kufanya kampeni za kuhamasisha umma kuhusu athari za kutumia dawa za kulevya.

 Naye  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema vita hiyo ni endelevu na serikali haitarajii  kushindwa.

Alisema serikali imejipanga pia kupambana na ubakaji, uhalifu wa kutumia silaha, ujangili na masuala ya ugaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles