NEW YORK, Marekani
SERIKALI ya nchi hii huenda ikayawekea vikwazo mataifa matano ambayo yanaendelea kununua mafuta kutoka Iran
Mataifa hayo ni pamoja na washirika wake Japan, Korea Kusini na Uturuki iwapo yataendelea kununua mafuta kutoka nchi hiyo.
Maofisa watatu wa serikali walisema juzi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo, anatarajiwa kutangaza kwamba serikali yake haitaongeza muda wa kuondolewa kwa vikwazo kwa mataifa hayo matano vitakapofikia muda wake wa mwisho Mei 2 mwaka huu.
Walisema mataifa mengine yanayokabiliwa na kitisho hicho ni China na India.
Hata hivyo haikuwekwa wazi iwapo miongoni mwa mataifa hayo matano yatapewa muda zaidi wa kumalizia ununuzi ama watakabiliwa na vikwazo hivyo vya Marekani vitakavyoanza Mei 3 kama hawatasimamisha mara moja kuagiza bidhaa hiyo kutoka Iran.