Na FRANCIS GODWIN- IRINGA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa, imewasainisha mikataba wakandarasi 14 kwa matengenezo ya barabara mbalimbali za mji wa Iringa.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Alex Kimbe, akizungumza jana kabla ya zoezi la kuwasainisha mikataba hiyo alisema kiasi cha shilingi 1,389,455,041.20 kimetengwa kwa kazi hiyo.
Alisema halmashauri yake imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya matengenezo na ujenzi wa barabara kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kupitia fedha za mfuko wa barabara.
“Kazi zinazokusudiwa kufanyika ni matengenezo ya muda maalumu (periodic maintenance works) ikihusisha ujenzi wa barabara ya lami ya Frelimo -Muungano (Routine maintenance works) na ujenzi /ukarabati wa madaraja.”
Alisema mchakato wa kuwapata wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ukifanyika kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 na kanuni zake na kuwa zabuni za ushindani kitaifa, zilitangazwa katika magazeti na website za zabuni ya mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma hivyo alitaka wakandarasi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Kimbe aliwataka wakandarasi hao kuanza utengenezaji wa barabara hizo na kuwa Manispaa haitasita kusitisha au kuvunja mkataba kwa mkandarasi atakayefanya kazi chini ya kiwango.
Kukamilika kwa miradi hiyo ya barabara kutarahisisha usafiri wa uhakika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa ambayo wananchi wake walikuwa wakisumbuka na adha ya usafiri kutokana na ubovu wa miundombinu.
“Kwa barabara kuboreshwa tutaboresha usafi wa mazingira, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya Iringa, pia kurahisisha utoaji na usimamizi wa huduma za jamii kama elimu na afya.”
Alisema kazi zitakazofanywa ni utengenezaji wa barabara ya kiwango cha lami barabara ya Frelimo na Muungano, pia matengenezo ya kawaida ya barabara za kata za Mtwivila, Nduli, Mlandege, Mshindo, Makorongoni, Kitanzini Isakalilo, Mvinjeni, Gangilonga, Ilala, Kitwilu, Ruaha, Mkwawa, Mkimbizi, Kihesa na maeneo mengine ya mji wa Iringa.