26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

BASATA KWA HILI MNASTAHILI PONGEZI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

JUMATATU wiki hii katika ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) uliopo Ilala Sharif Shamba, Dar es Salaam, kulifanyika hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa sekondari waliofanya vizuri kitaifa kwenye masomo ya sanaa.

Baraza kwa kutambua vipaji vichanga, wamerudisha mpango huo wa kuwatunuku wanafuzi wa kidato cha nne ambao mwaka jana kwenye mitihani yao walifanya vizuri katika masomo ya sanaa ya ufundi, maonyesho na muziki.

Mkakati huu wa kuwatunuku wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa kwenye masomo ya sanaa unakwenda kuimarisha imani ya wazazi kuwaruhusu watoto wao kupenda masomo yaliyo katika mchepuo wa sanaa.

Unajua sanaa yetu imekuwa na baadhi ya wasanii wachache ambao hawakujengewa misingi ya sanaa wanayoifanya toka wakiwa wadogo, ndiyo maana mwenendo wao umekuwa na mashaka makubwa hasa pale ambapo wanafanya kazi zinazokinzana na maadili ya mtanzania.

Tabia chafu zinazofanywa na vioo vyetu vya jamii zinatokana na wasanii hao kutokuwa na msingi mzuri tangu mwanzo. Mfano mzuri utaupata ukiwatazama wasanii wa filamu waliopita kwenye vikundi vya sanaa na wale walioingizwa kwenye filamu na urembo uliobebwa kwenye maumbo yao ya kibantu.

Sanaa imekuwa huru kiasi kwamba yeyote anaweza kufanya bila kusingatia weledi wake kisanaa, hiyo yote imekuja baada ya vipaji vichanga kukosa hamasa kama hii waliyoamua kuitoa Basata kwa wanafunzi.

Ndiyo maana baraza limeamua lianze kuwajenga wasanii wachanga wakiwa bado katika masomo yao ya sekondari ili wakue vyema kisanaa wakijua kuwa taa ya Basata inawamulika.

Katika tuzo za mwaka huu wanafunzi kutoka shule 5 za sekondari walitunukiwa, shule hizo ni Loyola, Azania za Dar es Salaam, Bukoba ya Mkoa wa Kagera, Darajani kutoka Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha Sekondari ya mkoani Arusha.

Natamani mwaka ujao tuzo hizi zitanue wigo wake na kuzifikia shule nyingi za Tanzania, maana naamini hii ni fursa kubwa kwa wanafunzi wengi wenye vipaji kuongeza juhudi katika masomo yao ili nao wapate nafasi ya kutunukiwa tuzo miaka ijayo.

Sehemu kubwa ya jamii yetu ilikuwa inapuuza sanaa licha ya mifano mingi ya watu waliofanikiwa kupitia sanaa za ufundi, maonyesho na muziki sasa nadhani tuzo hizi ni ujumbe tosha kwa wazazi, walimu na wanafunzi wenyewe kuwa masomo ya sanaa ni dili.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles