29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

MAJAMBAZI YATEKA MALORI MANNE, YAUA NA KUPORA 340,000/-

Na ABDALLAH AMIRI-IGUNGA

KUNDI la watu zaidi ya 15 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamefunga barabara kwa mawe na magogo kisha kuteka magari, kuwapora simu na fedha huku wakisababisha kifo cha dereva mmoja wa bajaji baada ya kumshambulia kwa silaha za jadi.

Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, linadaiwa kutokea saa 6:30 usiku katika barabara ya Dar es Salaam kwenye Kijiji cha Igogo Kata ya Nanga Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Akizungumza jana na waandishi wa habari akiwa amelazwa wodi No. 8 Hospitali ya Wilaya ya Igunga, mmoja wa madereva wa malori ambaye alitekwa, Ramadhani Bakari (34), alisema alifika hapo na gari lake akiwa anatokea Mwanza kwenda Iringa, alipofika hapo walikuta kukiwa na magogo hivyo wakati wakitafakari walivamiwa na kuanza kushambuliwa.

Alisema baada ya kutekwa waliamuriwa kushuka chini na kutoa fedha pamoja na simu, lakini wakati wakijiandaa kutoa fedha ndipo watu hayo walianza kumshambulia kwa marungu sehemu ya kichwa pamoja na panga hali iliyosababisha adondoke chini na kupoteza fahamu.

“Sikujua nini kiliendelea, ila nilishtuka na kujikuta nikiwa ndani ya gari yangu na milango ikiwa imefungwa lakini nilibaini simu zangu mbili pamoja na Sh 40,000 zilikuwa zimeibwa na watu hao,” alisema na kubainisha kuwa wakati huo askari walikuwa wamefika eneo hilo la tukio.

Mmoja wa waathirika alidai tukio hilo lilitumia dakika 20 ambapo majambazi hao walifanikiwa kuteka malori manne na bajaji moja ambapo dereva wake walimuua kwa kumshambulia kwa mapanga na marungu na kufanikiwa kutoweka na Sh 340,000 pamoja na simu za mkononi.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Igunga, Magongo Merchades, alieleza kupokea majeruhi wawili mmoja akiwa ni Charles Masanja aliyekuwa dereva wa bajaji na Ramadhani Bakari wa lori lakini mmoja alifariki kutokana na kuvuja damu nyingi.

Alisema Charles Masanja alifariki kutokana na majeraha makubwa kichwani na shingoni na kuongeza kuwa majeruhi mwingine bado amelazwa wodi No. 8 akiendelea na matibabu huku hali yake ikielezwa kuwa mbaya.

Akithibitisha kutokea kwa uvamizi huo, Mwaipopo alisema jumla ya malori manne yalitekwa na kuporwa kiasi cha fedha ambacho bado hakijajulikana.

“Polisi wanashughulika nalo jambo hili lakini nimeelezwa kuwa mbali na malori manne kutekwa pia waliteka na bajaji na kufanikiwa kumjerihi dereva wake ambaye alifariki wakati akiwa hospitali akipatiwa matibabu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Suleiman Issa, alipoulizwa kwa njia ya simu alisema yupo nje ya ofisi mkoani Dodoma kwa safari ya kikazi na kubainisha kuwa taarifa ya tukio hilo itatolewa ofisini kwake pindi watakapokamilisha taarifa za uchunguzi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles