Na MWANDISHI WETU
HALI ya taflani iliibuka jana baada ya Angeline Omina ambaye ni mama wa msichana aliyelelewa pamoja na mmoja wa pacha waliochanganywa kwenda kumchukua kwa nguvu mwanawe, Mevis Imbaya.
Tukio hilo limekuja baada ya siku chache mamlaka za nchini Kenya kutegua kitendawili cha pacha Sharon Mathius na Melon Lutenyo kufanana licha ya kutoka familia mbili tofauti
Matokeo ya vinasaba ambavyo vinaonyesha pacha hao ni ndugu kwa asilimia 99.9 yalikuja baada ya gumzo kutawala mitandaoni.
Msichana wa tatu Melvis Mbaya, ambaye alikuwa akilelewa na pacha mmoja wapo matokeo hayo yalionyesha si ndugu yao halisi wa kuzaliwa na hivyo kujenga hisia kwamba walichanganywa hospitalini miaka 19 iliyopita wakati walipozaliwa.
Omina ambaye ni mfanyabiashra ndogo ndogo wa Kangemi, Nairobi alikuwa amefuatana na maofisa watatu wa polisi wakati alipofika kumchukua mwanaye Mevis.
Huku akiwa amekasirika Omina aliishutumu familia ya mapacha hao kwa kumlazimisha binti yake, Mevis, kuendelea kuishi na Rosemary Onyango, ambaye ni mama wa mapacha hao na ambaye tangu akiwa kichanga nyumbani kwao Furfural, Kaunti ndogo ya Likuyani.
“Siwezi kubaki bila mtoto. hilo haliwezi kutokea,” alisikika akisema Omina.
Inaelezwa Omina alianzisha taflani hiyo wakati binti yake, Mevis, pamoja na wasichana hao pacha, Sharon Mathius na Melon Lutenyo na jamaa zao wakijindaa kukutana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.
Omina aliwashutumu ndugu wa pacha hao kwa kumshinikiza binti yake Mevis kuendelea kuishi na Rosemary Onyango, mama wa pacha hao huko Fufural.
Kabla ya ripoti ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) haijatoka wasichana hao walifanya uamuzi wa kuishi pamoja kama ndugu pasipo kushinikizwa.
Hata hivyo Omina anasema amebaini kuna nia ovu inayofanywa upande wa pili na ndio sababu ya yeye kutaka kuondoka na mwanae.
Pacha hao Sharon Mathius na Melon Lutenyo ambao wote ni watahiniwa wa kidato cha nne wamekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii
baada ya picha zao kuonekana hadharani wakiwa wamefanana licha ya kutoka katika familia mbili tofauti.
Matokeo ya DNA yalionyesha kuwa mama halisi wa pacha hao ni Rosemary Khaveleli Onyango wakibainika kuwa na chembechembe kwa asilimia 99.999.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya DNA hata hivyo yalionyesha Mevis ana chembechembe sawa kabisa na za Angeline Omina na Wilson Lutah Maruti yakithibitisha kwamba huyo ni mtoto wao.