24.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 16, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Tutahakikisha mkataba wa Bandari unazingatia maslahi ya Taifa

*Asema uwekezaji unafaida

*Atembelea bandari ya Mtwara, aagiza wanunuzi wa mikoa ya Kusini wachukue mafuta Mtwara

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uwekezaji una faida na kwamba suala hilo siyo kitu kipya.

“Uwekezaji una faida, hata hapa mbele yetu (jirani na eneo la mkutano) kuna eneo la bandari limekodishwa na mtu ameweka uzio. Hawa watu wanakodisha maeneo na wanayalipia,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Ijumaa, Julai 07, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Bandari, mjini Mtwara.

Amesema mwekezaji wa kwanza kwenye bandari ya Dar es Salaam ambako uwekezaji unapigiwa kelele, mkataba wake ulikuwa na vipengele vyenye mapungufu, vikaboreshwa mwaka 2017 na akaongezewa miaka mitano.

Akifafanua kuhusu makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya  DP World, Waziri Mkuu amesema:

“Ili mradi mmesema mkataba uzingatie maslahi ya Taifa, tutahakikisha mkataba huo unazingatia maslahi ya Taifa. Mmekuwa na hofu na ajira, hakuna atakayepoteza ajira. Mmekuwa na hofu na ardhi, kwamba anayekuja atachukua ardhi, siyo kweli. Hakuna mwekezaji aliyepewa ardhi kwa sababu hata kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha kukaa juu ya ardhi, na analipa kodi,” amesema Majaliwa na nkuongeza kuwa:

“Hofu nyingine ni muda wa mkataba, mmesema atakaa miaka 100. Hapana, haijatamkwa popote ila akija tutakubaliana miaka ya kukaa na kufanya tathmini kadri tunavyoona ukaaji huo utakuwa na maslahi ya Watanzania,” amesema.

Amesema kampuni ya DP World imewekeza kwenye nchi nyingi duniani na imejenga bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

“Mwekezaji huyu anahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ana meli zaidi ya 400. Meli hizi zitaleta mizigo kwenye bandari yetu. Ninawaomba Watanzania tumwamini Rais wetu, ana nia njema sana ya kiuchumi ya kufungua milango,’ amesema Majaliwa.

Mapema, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea bandari ya Mtwara na kukagua utendaji kazi wake ikiwemo gati mpya, flow meter na matenki ya kuhifadhia mafuta yanayomilikiwa na kampuni za GM na OILCOM.

Akiwa bandarini, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 300 umekamilika. 

“Gati hii ina uwezo wa kuhudumia meli hadi yenye uzito wa tani 65,000. Tumeongeza kina cha bandari hadi kufikia mita 13 na kazi yote iligharimu sh. bilioni 157,” amesema Mwakibete na kuongeza kuwa:

“Hivi sasa bandari hii ina uwezo wa kuhudumia tani  milioni moja za mizigo kwa mwaka kutoka 400, 000 kabla ya maboresho. Mwaka 2021/2022 kabla ya ujenzi wa gati hili, tulikuwa tunakusanya sh. bilioni 5 lakini mwaka fedha ulioisha wa 2022/2023, tumeweza kukusanya Sh bilioni 35.59. Tulikadiria kupokea meli 102 lakini tumeweza kupokea meli 313,” alisema. 

Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Norbert Kalembwe alisema bandari hiyo imenunua mashine mpya ya kupakua makontena kwenye meli kwa thamani ya sh. bilioni 90.

Alisema tangu Aprili mwaka huu hadi sasa, wamepokea makontena 4,600 yakiwemo yenye uwezo wa kuhifadhi vyakula ambayo yakifika bandarini hapo, yanaunganishwa na chaja za umeme ili kuendelea kutunza ubaridi uliomo ndani ya makontena hayo. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema wanaomiliki vituo vya mafuta Mtwara, Lindi na Ruvuma wanunue mafuta hayo kutoka Mtwara ili kuongeza kasi ya uchumi kwenye bandari hiyo.

“Nimeenda kwenye depot za GM na Oilcom, hawa ndugu zetu wamewekeza pale na tumewakodisha. Leo wamelalamika kuwa wauzaji wa rejareja hawachukui mafuta kutoka Mtwara.

“Wanaomiliki vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma hawana sababu ya kwenda Dar es Salaam kuchukua mafuta. Waje wachukulie Mtwara ili bandari yetu na yenyewe iwe inaleta meli za mafuta. Tusipofanya hivyo, tunaifanya bandari yetu isifanye kazi. Kama nilivyoagiza Tanga, Waziri mwenye dhamana akae na waliojenga matenki kwenye bandari ya Mtwara ili kuweka utaratibu ambao utawawezesha kufanya biashara. Hii itaongeza mzunguko wa fedha kwa wana-Mtwara,” amesema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles