26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Bomba la TAZAMA sasa kumlikwa upya

*Ulinzi zaidi kuimarishwa, wananchi kuhusishwa

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

TANZANIA na Zambia kwa pamoja zinatarajia kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayopitiwa na bomba la mafuta la TAZAMA ambalo kwa sasa linasafirisha dizeli badala ya mafuta ghafi.

Hayo yamebainishwa leo Dar es Salaam Ijumaa Julai 7, 2023 na Waziri wa Nishati, January Makamba, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi tangu kufanyika kwa kikao kilichokutanishwa mawaziri sita wa sekta za nishati na ulinzi kutoka Tanzania na Zambia.

Bomba la TAZAMA.

Kwa mujibu wa Waziri Makamba, maeneo mengine ambayo wamekubaliana ni kuongeza idadi ya askari watakaolinda bomba hilo, kushirikiana jamii zinazozunguka bomba hilo, ulinzi utaohusisha ndege zisizo na rubani maarufu kama ‘drone’ sambamba na kuongeza wigo wa bomba hilo ili kuliwezesha kusafirisha mafuta kwa kiwango kinachotakiwa tofauti na ilivyo hivi sasa.

“Katika mkutano wetu, tumekubaliana kuimarisha kamati za ulinzi na usalama ambapo bomba linapita, matumizi ya ndege zisizo na rubani na ushirikishaji wa wananchi katika vijiji vinavyopitiwa na bomba hilo.

“Smbamba na hayo tumekubalina kuimarisha miundombinu ikiwemo kambi na vituo vya polisi vinaongezeka katika maeneo yale ambayo bomba hilo linapita,” amesema Makamba na kuongeza kuwa kando ya eneo la ulinzi pia wamejadili juu ya upanuzi wa bomba hilo ili kusafirisha kwa ufanisi mafuta.

“Lakini pia tumejadili juu ya ujenzi wa bomba jipya la gesi,” amesema Makamba ambaye aliongoza kikao hicho.

Akitaja sababu za kuimarishwa zaidi kwa bomba hilo, Makamba amesema kuwa lilijengwa miaka 60 ambapo lilikuwa likisafirisha mafuta ghafi, lakini kuanzia Machi, mwaka huu limeanza kusafirisha dizeli  na siyo mafuta ghafi na kwamba kwa sababu hiyo lazima kuimarisha ulinzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Ambrose Lufuma, amesema wamekubaliana kuimarisha ulinzi katika bomba hilo, huku akisisitiza kuwa hivi sasa miundombinu hiyo inasafirisha bidhaa iliyochakatwa kwa ajili ya matumizi ya mwisho.

“Ifahamike tu kwamba hii ni bidhaa ambayo ipo tayari kwa matumizi hivyo inahitaji ulinzi wa kutosha. Hivyo tutahakikisha kuwa kunajengwa vituo vya polisi pembezoni mwa bomba hilo ili kuimarisha ulinzi,” amesmea.

Lufuma ameongeza kuwa iwapo ulinzi ukiimarishwa historia ya bomba hilo itaendelezwa, akisema mpango utakwenda sambamba kuongeza pia matumizi ya teknolojia katika usafirishaji nishati hiyo.

“Kutokana na uhitaji wa mafuta uliopo Zambia, tumepanga kuongeza wigo wa bomba la sasa kutoka inchi 8 hadi 12 na mpango wetu ni kufikia nchi 24, kwani tunaamini kwa kufanya hivyo kutasaidia kukabilianana mahitaji ya mafuta nchini kwetu,” amesema.

Mawaziri walioshiriki mkutano huo kwa upande wa Tanzania ni Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa, huku kwa Zambia wakiwa Waziri wa Nishati, Peter Kapala, Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacob Mwiimbu na Waziri wa Ulinzi, Ambrose Lufuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles