Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lugalo Kusiluka, amesema mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho yanaakisi mahitaji ya nchi kutokana na tafiti na bunifu mbalimbali zinazofanywa ambazo nyingi zimeleta matokeo chanya kwa jamii.
Profesa Kusiluka ameyasema hayo Julai 10,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) ambapo chuo hicho pia kinashiriki.
Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umevutia watu wengi kutokana na tafiti na bunifu zilizofanywa na chuo na matokeo yake kutangazwa kwa Watanzania.
“Tunashiriki kikamilifu katika maonesho haya kama sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na taifa letu za kuvutia biashara za aina mbalimbali na wawekezaji. Tunafundisha wataalam katika maeneo mbalimbali kama vile biashara, uchumi, ujasiriamali, masoko na mambo yote yanayohusiana na biashara, lakini biashara katika miaka ya siku hizi ni lazima uwe unajua kuifanya kisomi…miaka ya kubahatisha imeisha, sasa hivi tunafanya biashara kisasa,” amesema Profesa Kusiluka.
Profesa Kusiluka pia amewakaribisha Watanzania kwenda kusoma katika chuo hicho kwa sababu programu zote zinazofundishwa vyuo vingine wanazo.
Katika maonesho hayo chuo hicho kimeonesha bunifu katika mifumo mbalimbali ya kompyuta, lishe bora na lishe tiba kukabili magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ufugaji wa samaki, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Akili Mnemba na nyingine.
“Tumetembelewa na wahitimu wetu na kila aliyekuja ametoa taarifa nzuri ya kupokelewa alikokwenda, nasi imetupa nguvu kwamba wanafunzi tunaowaandaa wanakumbuka kwamba ndipo palipowajenga na wanawaambia wengine waje kusoma. Vitu ambavyo tunavifanya hatufanyi kwa maneno tu, tumeonyesha kwa vitendo na vinaonekana, tunaakisi mahitaji ya nchi,” amesema.
Aidha amesema chuo hicho ndio kilikuwa cha kwanza kutoa shahada katika lishe tiba na chakula hivyo uzoefu huo umesaidia wataalam kutengeneza vyakula mbalimbali na wana mpango wa kutafuta wadau na wabia waanze kutengeneza vyakula lishe ambayo ni tiba ili vipatikane kirahisi sokoni.
Amewataka wajasiariamali na wafanyabiashara wa vyakula wafike katika chuo hicho kwa kuwa wanazo formula za tiba lishe ili magonjwa yasiyoambukiza yapungue.
“Watu waje tushirikiane tutengeneze tiba lishe, Tanzania yenye afya ndiyo itakayotupeleka kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2050,” amesema.