24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mabadiliko ya tabianchi yagusa pato la Taifa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk.Seleman Jafo, amesema Tanzania inapoteza asilimia mbili hadi tatu ya pato la Taifa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Dk Jafo ameyasema hayo leo Desemba 18,2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia nchi (Cop28).

Mkutano huo uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12,2023 kwa lengo la kupitia taarifa, kufanya kutathmini, majadiliano na maamuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na nchi wanachama katika kufikia malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza kuwa kupitia mkutano huo Tanzania itanufaika zaidi na fedha za miradi, teknolojia, utaalam na programu mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo programu ya Afrika ya Nishati Safi ya Kupikia, programu ya afya na mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uhimili katika sekta ya maji, misitu na bahari.

Amesema Tanzania imeshiriki mikutano ya pembezoni ya ngazi ya juu iliyohusu uzinduzi wa mpango wa kukuza matumizi na nishati safi na nafuu ya kupikia kwa wanawake barani Afrika ulioshirikisha wadau 150.

“Pia kulikuwa na mkutano wa ngazi ya juu kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi , mkutano wa kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi katika sekta ya kilimo kwa kushughulikia hasara na uharibifu unaotokana na athari mabadiliko ya tabianchi ,” amesema.

Amesema masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni mikakati ya kukusanya Dola za Marekani bilioni 1.8 kwa ajili ya kuchimba visima 65,000 ambapo kila kisima kimoja kitahudumia wakulima wenye mashamba ya ukubwa wa hekta 2.5.

“Wadau wa maendeleo waliahidi kuchangia programu hii kiasi cha Dola za Marekani milioni 610,”amesema.

Amesema programu hiyo itasaidia uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya Kilimo na itapunguza uharibifu wa mazingira.

Aidha amesema kampuni na taasisi 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia mkutano Cop28.

“Wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania walikutana na wawekezaji kutoka nje ya nchi na kujadiliana kuhusu fursa za uwekezaji kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi ambapo jumla ya taasisi na kampuni zaidi ya 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini,”amesema Dk. Jafo.

Dk.Jafo amesema katika mkutano huo sekta binafsi na Asasi za Kiraia (AZAKI) 340 zilishiriki ipasavyo katika mkutano wa COP28 ikiwemo Benki ya Kilimo ya Taifa ambazo zilikuwa sehemu kubwa ya wajumbe wa Tanzania walioshiriki katika mkutano huo.

Amefafanua kuwa katika mkutano huo nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi zilikuwa na makubaliano 11 ambayo ilikuwa na lengo la pamoja la kuhimili hali hiyo.

Pia uendeshaji wa Mfuko wa kukabiliana na upotevu na uharibifu utokanao na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uundwaji wa bodi ya ushauri ya mfuko huo.

Aidha amesema mkutano wa 29 COP29 unatarajia kufanyika Azerbaijan Novemba 11 hadi 22, 2024 na mkutano wa 30 unatarajia kufanyaka nchini Brazil Novemba 10 hadi 21, 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles