MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema wanaompiga vita walie tu kwa sababu hawezi kuzuia mafuriko kwa mkono.
Lowassa ametoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Kashaulili vilivyoko Mpanda, mkoani Katavi. “Nilishasema siwezi kuzuia mafuriko haya kwa mkono, sasa yanawasumbua wao, nasema siwezi kuyazuia kwa mkono,” alisema Lowassa baada ya kupanda jukwaani na kushuhudia maelfu ya wananchi wa Mpanda waliohudhuria mkutano wake.
Akizungumzia operesheni tokomeza iliyofanyika nchini mwaka jana na kusababisha madhara kwa watu mbalimbali, Lowassa alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, ataunda tume kuchunguza operesheni hiyo ili kujua ni kwa nini Serikali haikuwalipa fidia waathirika.
“Mwaka jana Serikali iliunda Tume ya Operesheni Tokomeza, lakini najua bado kuna malalamiko kwa baadhi ya wananchi. “Wakati wa operesheni hiyo watu waliuawa, wapo waliofiwa, wengine walifilisiwa na hawakupewa fidia kwa madhara waliyoyapata.
“Kwahiyo, Mungu akinijalia nikaingia madarakani, nitaunda tume kuchunguza operesheni hiyo ili kujua ni kwanini wananchi hawakufidiwa. “Vilevile najua kuna mgogoro wa shamba la Efatha na wananchi ambapo wananchi wanasema ni shamba lao na mwekezaji huyo anasema ni mali yake.
“Kwahiyo, kama nitaingia madarakani, nitachunguza jambo hili kwa sababu haiwezekani mgogoro huo uchukue miaka mitatu bila ufumbuzi wakati mwenye mamlaka ya kuumaliza ni rais mwenyewe,” alisema Lowassa.
“Wawekezaji tunawahitaji, lakini lazima tuwalinde wakulima wadogo, kwahiyo nitachunguza kuona haki iko wapi. “Pia tutaunda tume kuchunguza mgogoro wa Bonde la Rukwa kwa sababu hatutaki migogoro ya wakulima na wafugaji iendelee kuwapo,” alisema.
Mwaka jana, Serikali ilianzisha Operesheni Tokomeza iliyolenga kukabiliana na uuaji wa wanyamapori wakiwamo faru na tembo uliokuwa umekithiri nchini. Baada ya operesheni hiyo kuanzishwa, washiriki waliendesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo baadhi ya watu waliuawa, wengine walipata ulemavu wa kudumu na baadhi walipoteza mali zao katika mazingira yasiyokubalika.
Kutokana na hali hiyo, Bunge liliiagiza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, ichunguze jinsi operesheni hiyo ilivyotekelezwa.
Baada ya uchunguzi wa kamati hiyo na ripoti kuwasilishwa bungeni, mawaziri wanne walitenguliwa uteuzi wao baada ya kuonekana walishindwa kutimiza wajibu wao wakati wa operesheni hiyo.
Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Mathayo David.
MBOWE
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipokuwa akihutubia mkutano huo, alisema safari yao ya kuingia madarakani, imerahisishwa na Lowassa kwa kuwa wananchi wengi wanamuunga mkono.
“Safari yetu ya mageuzi ilikuwa kama safari ya treni ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma. Baada ya kumpata Lowassa, sasa safari yetu ni nyepesi, lakini tunaomba Watanzania mtuunge mkono kwa sababu bado ina vikwazo.
“Nyota ya uongozi kwa Lowassa ilikuwa ya miaka mingi ila CCM hawakujua kama anapendwa na wananchi ndiyo maana wakampuuza, wakamkejeli na kumsemea uongo.
“Kwahiyo, naomba wana mageuzi tusiwatukane walioko CCM kwani wapo watakaotusaidia kama ilivyo kwa Lowassa,” alisema Mbowe.
Pamoja na hayo, aliwasisitizia Watanzania umuhimu wa kuwachagua wagombea wote wa Ukawa ili wasaidie kuleta maendeleo nchini.
MGEJA
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema ni aibu kwa Serikali ya CCM iliyokaa madarakani kwa miaka 50, kuendelea kuomba misaada kutoka kwa wafadhili.
Pamoja na hayo, alisema CCM haina sababu ya kuendelea kuomba ridhaa ya kuiongoza Tanzania kwa kuwa imejaa walarushwa.
“CCM imejaa wala rushwa na kutokana na mfumo huo, ndiyo maana wanapokaa hawajadili masuala ya wananchi na badala yake wamekuwa wakijadili masuala yao binafsi.
“Kuna wana CCM wamekuwa wakisema hawawezi kukihama chama chao, lakini nawaambia CCM ni kama nyumba inayoungua na kinachotakiwa sasa ni wao kuhama na kujiunga na Ukawa.
“Kwahiyo, nawaambia tena, mgombea wa CCM ndugu Magufuli hafai kuwa rais wa nchi hii, kwani ni mbabe na ndiye amekuwa akivunja nyumba za watu bila kuwalipa fidia,” alisema Mgeja.