22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

kada CCM akiri kuhusika na Chadema ‘feki’

masaburiNA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Didas Masaburi, amekiri kukutana na vijana wanaodaiwa kujifanya wafuasi wa Chadema walioandamana jijini Dar es Salaam kupongeza hatua ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuacha siasa na kushambulia chama chake.

Juzi vijana hao waliandamana wakiwa na lengo la kwenda makao makuu ya Chadema kabla ya kutawanywa na wananchi.

Tangu asubuhi ya jana, sauti ya Masaburi ilikuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii akisikika akiwapongeza vijana hao baada ya maandamano yao kutofikia lengo na baadhi yao kukamatwa na polisi.

Ilipofika mchana, Masaburi aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kukiri kukutana na vijana hao na kuwapongeza kwa kuandamana kwao.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya vijana hao kutawanywa juzi, baadhi ya viongozi wa Chadema Jimbo la Ubungo, walisema maandamano hayo yaliratibiwa na Masaburi aliyechukua vijana mtaani na kuwavalisha fulana za chama hicho ili waandamane wakijifanya ni wafuasi wa chama hicho.

Jana, Masaburi alisema hata yeye binafsi angekuwa Chadema angeandamana kuunga mkono hoja zilizotolewa na Dk. Slaa.

“Mimi binafsi niliwaunga mkono vijana baada ya maandamano, lakini sikuwatuma waandamane. Pia nilisema kuwa vijana wa Chadema wanaorudi CCM viongozi wote watawaunga mkono.

“Hata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akija CCM nitamuunga mkono na nitamkaribisha vizuri,” alisema Masaburi.

 

SAUTI YA MASABURI

Sauti hiyo ya Masaburi iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii, inasikika ikisema: “Vijana waliotokea upande wa Ubungo na waliotokea Mwenge walikuwa hawaonekani ikaonekana hakuna kilichoendelea ndio maana mlipata shida.

“Lakini siwakatishi tamaa, ni impact (matokeo) kubwa, hata Kinana, Magufuli na Rais mwenyewe anajua kinachoendelea, na hakuna vijana walioongoza vizuri kama Kimara, wameonekana wana uchungu na CCM, wanahitaji, naomba muendelee na moyo huo, inabidi tuwaandalie vijana wa Kimara wali pamoja na vijana wengine.

“Hata jana niliwaambia vijana hawa (waratibu wa maandamano hayo) itakuwaje, aliniambia wapo vijana wengi wa kujitolea na wapo zaidi ya 200 nikajua nitapata hata 20. Vijana 218 idadi hiyo ni kubwa sana, tunawaomba muendelee na moyo huo huo.”

Sauti ya mmoja wa vijana waliokuwapo ikajibu: “Vijana wengi walijitolea na walikuwa wengi sana, lakini baada ya vurugu kutokea wengi walitawanyika na kuondoka nyumbani.

“Wengi wameondoka nyumbani, na wengine ndio hapo wapo polisi, wapo sita, yaani wengi sana wameondoka wameenda nyumbani.”

Ikasikika tena sauti ya Masaburi: “Wote hao muwaambie mheshimiwa mbunge mtarajiwa amewashukuru sana, na anasema lazima tuendelee kushiriki (maandamano), lazima mtaona impact yake na lazima tuendelee na jitihada hizi kwa sababu tusipofanya hivyo, wale wanaojiita wana foo wanaweza wakatushinda, hivyo lazima tuwaonyeshe kuwa nyie ni wezi, mafisadi hata wenzenu wa Chadema hawawataki.

“Ndiyo maana sisi tunaimba hatukutukutu… hatukutaki mnajua huo wimbo?”

Sauti ya vijana ikasikika: “Hatukutaki umepotea na Chama cha Chadema.”

Kisha inasikika sauti ya mmoja wa vijana: “Mimi nilikuwa na wimbo mpya kidogo ‘Chadema tunahama.. Chadema tunahama…, Slaa kasema kweli… Slaa kasema kweli.” Akaongeza: “Hii ni hoja mpya iliyokuwepo leo.”

KIjana mwingine: “Hata waandishi wa habari walikuja baada ya watu kukamatwa kamatwa.”

“Walichelewa kidogo,” anasikika kijana mwingine.

Mwingine anadakia: “Hawakuchelewa walikuja wakaondoka.”

Sauti ya kijana mwingine wa kike inasikika: “Yupo mwandishi wa habari alikuja na gari yake akasimama akasema ninyi mtakuwa mmetumwa na CCM tukasema hapana, akasema njoo basi tuongee hapa pembeni tukasema hapana ngoja tuongee ukweli wakasema basi ninyi mtakuwa mmetumwa. Mara wakasema njoni nyie watatu  na viongozi wenu mliokuja nao tukakataa. Kuna mtu mmoja alikuwa na kadi ya Chadema akaonyesha, dada mwingine akaja akanisukuma pembeni, akakamatwa, naona ndani kuna wengine wamewekwa pembeni, naona wengine wanatoka, nikaona hapa hapakaliki.”

Kisha inasikika tena sauti ya Masaburi: “Kosa lingine ambalo tulilifanya sisi na tumejifunza  ni kwamba  hatukuweka askari wetu wale wa kejeli.”

Kijana mwingine anadakia: “Hata sisi tulikuwa na msimamo, tulikuwa tumejipanga wenyewe, pia tuliwaambia askari wapo, na mwingine akasema mbona siwaoni askari hapa nikaanza.”

Inasikika sauti ya kijana wa kike: “Wapo watu walikuwa makaburini walikuwa wamejificha.”

Kisha inasikika tena sauti ya Masaburi: “Pale makaburini walikuwepo watu karibu na magari, wale ni fundi magari wanatengeneza karibu na makaburi, lakini ni wanachama wa Chadema.”

Anasikika kijana mwingine: “Yaaani safari nyingine tunatakiwa tuwe na kadi za Chadema, wakati tupo kule ndani tuliulizwa kadi ziko wapi kwa sababu tungekuwa nazo aaaaaa, una kadi ya CCM halafu unahojiwa unashindwa kujieleza.

“Tungekuwa na kadi tungeweza kujieleza. Kijana mmoja aliingia akajitoa muhanga nikamwambia aangalie hakuna mtu wetu aliyebaki huko wakati tunawasiliana na wewe, mimi polisi si tatizo, tatizo  langu ni kubaki mle ndani, anaweza akamnyonga mtu. Mimi najulikana sana mle ndani.”

Akasikika tena Masaburi: “Mimi nimemwambia mheshimiwa nije niwasalimu na zawadi yangu kubwa ninayoweza kuwapa ni kuwashukuruni na kuwatia moyo tuendelee na  moyo huo huo ndio CCM itakuwa chama.

“Maana yake wale wanafanya mambo kama haya haya wanaandamana hivi,  unaonaje tena kwa nguvu zote  wakiimba kwa nguvu zote na kuruka ruka Lowassa… Lowassa…. na sisi CCM tusipofanya hivyo hatuwezi kwenda mbali, lazima na sisi tuamke tujibadilishe wenyewe ili tuweze kuendeleza chama chetu.

“Mimi sina mengi zaidi ya haya, lengo langu ni kuwasalimu, kuwashukuru na kuwaambia watu tupo pamoja na kupata majina ili tuweze kuwajua.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles