24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Padri mtarajiwa akamatwa kwa mauaji Arusha

LiberatusSabasNA JANETH MUSHI, ARUSHA

JESHI la Polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tano wa masomo ya falsafa katika Chuo cha Dini cha Kanisa Katoliki kilichopo Segerea, Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji.

Elijus Lyatuu (31), anashikiliwa kwa tuhuma za kumuua Alfred Kimbaa (18) maarufu kwa jina la Mandela mwanzoni mwa wiki katika Hoteli ya A Square Belmont katikati ya Jiji la Arusha.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa alimuua Kimbaa usiku wa kuamkia Jumatatu katika hoteli hiyo na kuchukua baadhi ya viungo vyake vya mwili kikiwamo kichwa, sehemu za siri, matiti na viganja vya mikono.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema  mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba mosi mwaka huu katika barabara ya Makongoro eneo la TRA jirani na Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Kamanda Sabas alisema upelelezi uliofanywa na jeshi hilo uliwezesha kumkamata Lyatuu ambaye aliwasili jijini Arusha wiki mbili zilizopita na kufikia nyumbani kwa Kimbaa eneo la Mianzini na walikuwa wanaishi chumba kimoja ila ilitokea sintofahamu kati yao kiasi cha kushindwa kuelewana.

Alisema viungo vya mwili wa marehemu vimepatikana katika eneo la Mto Misheni, Usa River, baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa na polisi na kuwapeleka katika eneo hilo alikokuwa ameviweka.

Kamanda Sabas alisema siku ya tukio Lyatuu na Kimbaa walikuwa hotelini hapo ili kusuluhisha tofauti zao, lakini wakashindwa kuafikiana na ndipo mtuhumiwa akamuua mwenzake.

“Mtuhumiwa alifika Arusha wiki mbili zilizopita na akawa amefikia nyumbani kwa Kimbaa kwa vile ni watu wanaofahamiana ikizingatiwa mtuhumiwa ni ndugu wa mmiliki wa duka alilokuwa akifanya kazi Kimbaa na wakawa wanaishi chumba kimoja.

“Lakini kulitokea kutokuelewana kati yao na katika kutokuelewana huko ndipo mtuhumiwa akafikia hatua ya kumuua mwenzake,” alisema Kamanda Sabas na kuongeza:

“Pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, pia kumeweza kupatikana vielelezo vyote, yaani viungo vya marehemu baada ya mtuhumiwa kuwapeleka  polisi kule alipovitupa Mto Misheni…upelelezi unakamilika ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.”

Kamanda Sabas alipoulizwa kuhusu chanzo cha Kimbaa na Lyatuu kutokuelewana, hakuwa tayari kuzungumzia mgogoro kati yao, akisema kuwa mambo mengine yataenda kujulikana mahakamani mtuhumiwa huyo atakapopelekwa kujibu mashtaka yanayomkabili.

Inadaiwa kuwa chanzo cha sintofahamu kati ya Kimbaa na mtuhumiwa huyo ni fedha.  Inaelezwa kuwa mtuhumiwa kabla ya kufanya mauaji hayo aliachiwa ufunguo wa duka hilo na Mandela na baada ya kurudi dukani alikuta  zaidi ya Sh milioni 10 zikiwa hazipo.

Vyanzo vya habari vilieleza kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuulizwa zilipo fedha hizo alimtaka Kimbaa waende hotelini wakazungumze.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles