27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa Dk. Slaa Amwaga mboga

mke wa slaaAZIZA MASOUD NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

KWA vijana wa mjini, wanaweza kusema  kwamba alichofanya Dk. Willibrod Slaa juzi kwa kuachana na siasa na kurusha tuhuma kwa chama chake, ni sawa na kumwaga ugali, na majibu aliyotoa mkewe wa kwanza, Rose Kamili jana, ni sawa na kumwaga mboga.

Mke huyo aliyedai kutelekezwa na Dk. Slaa mwaka 2010 pamoja na watoto, alisema kiongozi huyo ni mwongo na ni dhaifu kwa wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rose alisema ameshtushwa na kauli zilizotolewa na Dk. Slaa, na hasa zile zilizoelekezwa kwake moja kwa moja na familia yake.

Rose ambaye ni mke wa ndoa wa kiongozi huyo wa zamani wa Chadema, alisema kauli Dk. Slaa kuwa familia yake imekuwa ikishindia mihogo kwa sababu ya kuhangaikia na Chadema, ni kiashiria cha uongo wa wazi.

“Siwezi kusema kwamba mihogo ni mibaya kuliwa, lakini napenda kukiri kwamba katika maisha yetu niliyokaa na Dk. Slaa kuanzia mwaka 1986, sikuwahi kushuhudia familia yetu ikila mihogo kwa sababu ya kukosa chakula kama alivyosema kwenye hotuba yake,” alisema.

Aliongeza kuwa hata kauli yake kwamba Serikali ilimwekea pingamizi ili asifunge ndoa na mchumba aliye naye sasa, Josephine Mushumbusi, ni uongo kwani ni yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwa sababu ni mkewe rasmi wa ndoa.

“Jambo la kujiuliza hapa ni kwamba tangu lini Serikali ikaweka pingamizi wakati aliyepinga ni mkewe. Ukweli ni kwamba mimi ndiye niliyeweka pingamizi hilo ili kunusuru kunyang’anywa nyumba na hatimaye kuhangaika na watoto,” alisema.

Kuhusu kauli ya Dk. Slaa kwamba anamchukia Lowassa na hajazungumza naye kwa muda mrefu, Rose alisema waziri mkuu huyo wa zamani, ndiye aliyemshauri kuhamia Chadema mwaka 1995 na kugombea ubunge wa Karatu baada ya jina lake kukatwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.

“Nakumbuka wakati tukizungumzia suala hilo ilikuwa jioni na tulikwenda nyumbani kwa Lowassa, Monduli baada ya jina lake kukatwa na CCM, ndiyo akamshauri kuhamia chama kingine, sasa hizo chuki zinatoka wapi?” alisema na kuhoji.

Kuhusu Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Rose alisema pia ni uongo mwingine kwa sababu wawili hao walipigiana simu na kufanya mazungumzo wiki iliyopita.

“Kwanini aonyeshe chuki na watu wakati sisi ametutelekeza kwa muda mrefu, lakini tumekuwa tukimlinda? Sasa inashangaza ni kwa nini padri huyu mstaafu anaonyesha chuki kwa wengine,” alisema.

Aidha Rose pia alionyesha kusikitikia hatua ya mumewe kuzusha maneno ya uongo kwa viongozi wa dini, akiwatuhumu kuhongwa zaidi ya shilingi milioni 60 na Lowassa ili wamuunge mkono.

Pia alisema kumuhusisha Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kwamba ndiye alimleta Lowassa Chadema ni kichekesho kwa sababu muunganishaji mkubwa wa suala hilo ni yeye (Dk. Slaa) ambaye anasali katika kanisa hilo.

Uongo mwingine alioutaja mkewe huyo wa ndoa ni kuhusu kukataa kwake kutojiandaa kuwania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati inajulikana kuwa alikuwa akifanya maandalizi ndani na nje ya nchi kwa ajili ya suala hilo.

Rose aliendelea kubainisha kuwa tatizo kubwa la mumewe ni kuzungumza mambo kwa kukurupuka na kutokuvumilia, na hata kudiriki kutoa siri za viongozi wenzake waliokuwa wakimtaka arudi ofisini.

“Aliniambia kwamba alikuwa akifuatwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyemuahidi kwamba iwapo atakaa kimya atateuliwa kuwa mbunge na baadaye kuwa waziri, akaniambia Rais Kikwete alimuahidi kumpatia ubalozi, ikiwamo na kuitwa na Kardinali Pengo ambaye hakusema walizungumza jambo gani.

“Maneno hayo nimekuwa nikiyapata kutokana na tabia ya Dk. Slaa kwa kutokuwa na mdomo na ulimi usiokuwa na mfupa, hivyo kila jambo analoelezwa huwa analiweka wazi, na inawezekana safari aliyokwenda Afrika Kusini baada ya kumalizika kikao ndiyo kaelekea Ubalozi wa Afrika Kusini,” alisema Rose.

Rose alipasha kwamba Dk. Slaa ambaye amekuwa akimfahamu, amekuwa tofauti na huyu aliyemsikia akizungumza kwenye mkutano ule na hilo limetokana na udhaifu mkubwa alionao kwa wanawake.

“Dk. Slaa siye ninayemjua, anaonekana anaendeshwa na mwanamke aliye naye na ndiyo maana hata alikubali kumleta Lowassa kwa asilimia 80, lakini alipofika nyumbani alibadili msimamo baada ya kulazwa nje ya nyumba yake,” alisema.

Rose ambaye ni mbunge wa viti maalumu (Chadema) aliyemaliza muda wake, alisema amekuwa akiwasiliana na mumewe huyo kwa muda mrefu, na hata alipopata taarifa za kugoma kwenda ofisi za Chadema, wanawe walikwenda nyumbani kwa Dk. Slaa kumjulia hali.

“Cha kushangaza ni kwamba watoto walivyofika nyumbani kwake walibisha hodi, lakini walizuiliwa ndipo babu yao (baba yake Dk. Slaa) ndiye alitoka na kuzungumza nao nje ya geti huko JKT Mbweni,” alisema Rose aliyeambatana na watoto wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles