KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam kesho inatarajia kuanza kusikiliza maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anayeitaka pamoja na mambo mengine itoe zuio la kumwapisha mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu na ruhusa ya kumshtaki Spika Job Ndugai kwa kumvua ubunge bila sababu za msingi.
Wakati mahakama ikitarajiwa kuanza kusikiliza maombi hayo, tayari ratiba ndogo ya mkutano wa 16 wa Bunge unaotarajia kuanza kesho kutwa, inaonyesha Bunge litaanza na shughuli ya kiapo cha uaminifu.
Kiapo hicho cha uaminifu kwa kawaida huwagusa wabunge wapya baada ya kuanza kwa kikao chao cha kwanza bungeni.
Kwa sababu hiyo, anayeguswa na ratiba hiyo ni mrithi wa Lissu, ambaye ni mbunge huyo mteule wa Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mtaturu.
Hatma ya kuapishwa au kutoapishwa kwa Mtaturu kesho kutwa itajulikana zaidi kesho baada ya maombi hayo kuanza kusikilizwa na mahakama.
Kinachosubiriwa kwa hamu na wadau mbalimbali wakiwamo wa sheria, ni mihimili hiyo, Bunge na Mahakama – kila upande utakavyoheshimu maamuzi.
Maombi hayo yamefikia hatua ya kusikilizwa baada ya mahakama hiyo kuyatupilia mbali mapingamizi ya Jamhuri kutokana na kile ilichoeleza kuwa hawakuwa na hoja za msingi za kufanya shauri hilo lisisikilizwe.
Mapingamizi yalitupwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kukubaliana na hoja za Wakili wa Lissu, Peter Kibatala, kwamba hoja zao hazina msingi.
Lissu pamoja na mambo mengine, anaomba zuio la muda la kuapishwa Mtaturu.
Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa
kaka yake, Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Maombi hayo ni dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.
Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo, impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe taarifa yake ya kumvua ubunge.
Anaiomba mahakama hiyo itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge kwa sababu alikuwa akijua kwamba alipigwa risasi na yuko kwenye matibabu.
Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.
Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.
Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.
Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Hata hivyo Spika Ndugai alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni Katiba ya nchi.