31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ndege iliyozuiwa Afrika Kusini ‘kula vichwa vya watu’

Mwandishi wetu-Dodoma

MSEMAJI wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, amesema watakaobainika kuihujumu nchi kupitia kuzuiwa kwa ndege ya Serikali nchini Afrika Kusini watafunguliwa kesi ya kuhujumu nchi.

Dk. Abbas alisema watu hao watafunguliwa mashtaka hayo baada ya kumalizika kesi ya kuzuiwa kwa ndege hiyo inayosikilizwa katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ya Gauteng.

Kauli hiyo imekuja baada ya juzi jopo la wanasheria kutoka Tanzania kuanza kupinga  uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Afrika Kusini wa kuizuia ndege hiyo ya Serikali inayotumiwa na Shirika la Ndege la ATCL.

Ndege hiyo ilizuiwa kuruka Uwanja wa Ndege wa OR Tambo jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 23, mwaka huu kwa zuio la mahakama  baada ya shauri la awali kumpa tuzo mkulima mstaafu, Hermanus Steyn anayeidai Serikali Dola za Marekani milioni takribani 30.

Steyn, mzungu ambaye alikuwa akiishi Tanzania kabla ya kutangazwa kuwa ni mhamiaji haramu, anadai fedha hizo kama fidia baada ya mali zake, ikiwamo kampuni yake ya Rift Valley Seed Limited, shamba, vifaa, magari 250 na ndege ndogo 12 kutaifishwa Januari 1982.

Hata hivyo, juzi jopo hilo la mawakili wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi, waliiambia Mahakama ya Gauteng kuwa yalifanyika makosa katika utoaji wa amri ya kuikamata ndege hiyo.

Mahakama inasubiriwa kutoa uamuzi wa ama kuiachia au kutoiachia ndege hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili.

Akizungumza Dodoma jana, Dk. Abbas alisema wapo Watanzania wanaoshiriki kuihujumu Serikali kupitia  ndege hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 90.

“Wapo wazawa wanaofanya mawili matatu kuhujumu nchi, lakini niwaeleze tusubiri kesi iishe huko Afrika Kusini, tutawafungulia kesi ya kuhujumu nchi yetu.

“Hakuna nabii katika historia ya manabii aliyewahi kuaminiwa kwa asilimia 100, hivyo huwezi kukubaliwa na watu wote.

“Hata hii ndege inayoshikiliwa ikija Tanzania ipo siku wanaochukia watatumia usafiri huo kwenda Afrika Kusini, kama sio wao basi watoto wao,” alisema Dk. Abbas.

Alisema mawakili wa Serikali wameshawasilisha hoja tatu Mahakama Kuu ya Gauteng nchini humo.

Dk. Abbas alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni hukumu, hivyo ana imani ndege hiyo itarejeshwa nchini.

“Pamoja na changamoto mbalimbali za baadhi ya Watanzania kushirikiana na mawakala wengine wa nje kutaka kuihujumu nchi yetu kama mlivyosikia, suala la kushikwa ndege zetu au kutumia baadhi ya majarida kujaribu kuichafua nchi, heshima na hadhi ya Tanzania kimataifa imeendelea kupanda kutokana na nia njema ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Dk. John Magufuli,” alisema Dk. Abbas.

Ndege hiyo ilishikiliwa kutokana na maombi namba 28/994/2019 yaliyowasilishwa na mwombaji Steyn kupitia ofisi ya uwakili ya Werksmans iliyopo nchini humo.

Maombi hayo ya kusikilizwa upande mmoja yaliwasilishwa Agosti 21, mwaka huu dhidi ya Serikali ya Tanzania, Uwanja wa Ndege wa Afrika Kusini, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Afrika Kusini, Kampuni ya Ndege Tanzania, Sibusisi Nkabinde, Kgomotso Molefi na Patrick Sithole.

Katika maombi hayo kuliambatanishwa na kiapo kilichoapwa na Martin Richard Steyn na Bianka Pretorius, wakisapoti maombi ya kushikilia ndege kwa sababu mdai anadai Serikali ya Tanzania Dola za Marekani 36,375,672.81.

Mahakama ilisikiliza maombi hayo upande mmoja na tarehe hiyo hiyo yaliyowasilishwa na kukubali hoja za mwombaji na kuamuru ndege ikamatwe.

Mwaka 2010 mbele ya Jaji Mstaafu Josephat Manckanja, mdai alikuwa anadai fidia ya shamba lake jumla ya Dola za Marekani milioni 36.

Mahakama ilikataa, pande zote mbili wakaketi kwa makubaliano na walifikia makubaliano ya Serikali ya Tanzania kulipa Dola za Marekani milioni 30.

Baada ya makubaliano hayo, inaelezwa Serikali ya Tanzania ilianza kulipa na ilishalipa kiasi kikubwa cha fedha.

Taarifa zinaeleza pamoja na kuwa tayari malipo yalishafanyika kwa kiasi kikubwa, mdai katika maombi yake anadai kiwango kile kile cha awali cha zaidi ya Dola za Marekani milioni 36 kilichokuwepo kabla ya makubaliano.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles