TASWIRA za Wanaughaibuni zinatuponza, wengi wanafikiria kwamba tunao uwezo mkubwa, lakini hawaoni uwezo huo umetokana na miaka mingi ya kazi na kujinyima. Miaka mingi ya kuishi na kufanya kazi kwenye mazingira magumu yametufanya tuheshimu kazi na kuelewa kwamba, hata kama mchango ni mdogo lakini kila senti inahitajika mara mia mbili na zaidi.
Kwa bahati mbaya vyombo vya habari na hasa filamu zimewapoteza wengi katika kupata habari ambazo si za kweli, vijana wengi hawaelewi wanavyoviona kutokana na kuangalia katika mazingira ambayo hayafanani na kule picha hizo zinatengenezwa. Dhana ya watu kupata utajiri wa haraka Ulaya umeshika hatamu.
Ni jambo la kusikitisha mawazo yote yapo hapo kufikiria kwamba msaada wa kujiwezesha utatoka Ughaibuni. Hii inatupotezea malengo na kutokuona uwezo wa kujiendeleza upo hapo ulipo.
Kuweza kusaidia nyumbani ni heshima kubwa na ni wajibu wetu. Kuwa na moyo wa kusaidia ni sehemu ya utamaduni wetu wa Kitanzania. Utamaduni huo umeleta na ufahamu kuwa sisi ni watu wamoja na tuko tayari kutambulika kama taifa moja, aidha sasa au katika siku za nyuma. Kwa siku hizi unapigwa vita kwa sababu baadhi ya watu wanaona kwamba ubinafsi ndio msingi na sio undugu na ujamaa. Utamaduni wetu umeshindwa kuingiliana na kujiunganisha na maendeleo ya sasa, umekosa tafisiri kwa mazingira ya kisasa.
Huu utamaduni umeanza kuzorota na kumomonyoka kwa watu kushindwa kuelewa na kupata miundombinu ya kuunganisha utamaduni wa Kiswahili na jamii ya kisasa. . Katika kuukumbatia utamaduni unaokuja na jamii ya kisasa tumeacha mambo mengi ya msingi ambayo ni pamoja na kujitegemea.
Utakuta mara nyingi watu wanategemea ndugu na jamaa wawaangalie na kuwasaidia kutatua matatizo yao  bila wao kujishughlisha kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao na hii inasababishwa kwa upande mwingine kutokuelewa kwa upana dhana ya ubepari.
Ukosefu wa kutotengeneza mazingira ya kupokea fikra unaoendana na utamaduni nje ya jamii ya utamaduni wa Kiswahili, kutokuelewa huko kumetudumaza.
Katika utamaduni wetu kuna mchanganyo wa kila kitu, kuanzia biashara mpaka siasa. Ndani ya huo utamaduni kunapatikana demokrasia ambayo imeunganishwa katika kila matawi. Sasa katika kuchukua fikra za watu ambao hawaelewi jinsi jamii yetu ilivyokuwa, kufungama na kuingiliana katika shughuli zote kupitia biashara, kumeleta mgongano wa fikra na falsafa.
Na hali hii inachanganyika zaidi na ushindani mwingi wa kisiasa. Sio kwamba kuna ubaya wa ushindani ila ni njia zinazotumika katika kutafuta kuongoza jamii.
Huu utamaduni wetu umepotea kwa sababu ya ubinafsi ambao umeingia katika mzingira yetu. Ubinafsi huu umeletwa katika makosa ya kutafsiri maana ya ubepari kwa Kiswahili. Sasa tafsiri polepole inaanza kueleweka. Ubepari sio ubaya kwa aina yoyote, kwenye ubepari kuna ujasiriamali.
Wasomi hawakufafanua vizuri maana ya ubepari na katika hayo makosa yameingia kwenye jamii yetu na kuwapumbaza kwa kutokuchukua nafasi ya mbele ya kujiendeleza na kujiajiri
Utamaduni wa Ughaibuni ni muhimu sana kujitegemea na kama hujitegemei basi tafuta ajira. Kwa sisi ambao tumekuja huku na kutafuta maisha umekuwa ni sehemu ya maisha yetu.
Tukija nyumbani tunajaribu sana kuwaelimisha wenzetu. Kwa sababu ya urasimu na mazingra ya watu ambao bado wanaona ni haki wapate msaada bila ya kujitahidi kujiondoa katika hali ngumu basi elimu hii imechelewa sana.
Ughaibuni au Ulaya Magharibi kuna baadhi ya utaratibu ambao Watanzania tunaweza kuingiza kwenye utamaduni wetu. Sio kila kitu tunaweza kuiga ni baadhi tu. Vinginevyo vinaweza kupatikana kwenye utamaduni wetu wa mpaka vile tunavyofanya biashara, kwani hii imekuwa toka enzi za ujenzi wa jamii za Kiswahili.
Mambo mengi yamechangia kutokuelewa kwamba ubebari sio mbaya ila ni njia moja ya kupata ajira na kujiendeleza, ni ujasirimali. Nchi yetu Tanzania ina rasilimali nyingi sana na bado kuna nafasi nyingi sana za kujiendeleza bila ya kutegemea au kuwa mzigo katika jamii, kuweka miundombinu ya kusaidia ndugu na jamaa iwe ni moja ya mikakati ya wanaoongoza jamii zetu. Mikakati isitoke juu tu bali pia itoke hata kutoka kwenye Serikali za mitaa. Ujengaji wa jamii na maendeleo ukiletwa na uendelevu bora wa asili ya hiyo jamii utaepukana na matatizo ya kutafsiri fikra ambazo sio za asili hiyo na kutengeneza kiunganisha cha asili ya Magharibi.
Kiswahili ni lugha ambayo inabeba mila na desturi ambazo zipo kwenye jamii nyingi nchini na nje ya nchi. Kuendeleza Uswahili wetu bila ya kuingiza maana mbaya ni jambao ambalo linaweza kututoa katika malumbano madogo madogo ambayo yatatupotezea muda na yanachukua nguvu kubwa sana.
Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga.