24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP KUIONDOA MAREKANI MAKUBALIANO BIASHARA HURIA

WASHINGTON, MAREKANI


donald-trump

RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump, amesema ataiondoa nchi yake kutoka Ubia wa Biashara Huria na Mataifa ya Asia (TTP) katika siku yake ya kwanza akiingia madarakani.

Katika ujumbe alioutoa kwa video akiainisha mambo muhimu atakayoshughulikia katika siku 100 za kwanza madarakani, Trump aliyakosoa makubaliano ya mataifa 12 ya eneo la Bahari ya Pasifiki.

Mataifa hayo yakizihusisha Malaysia, Australia, New Zealand, Canada, Mexico na Japan kwa pamoja yanadhibiti asilimia 40 ya uchumi wa dunia.

Trump ambaye anatarajiwa kuingia madarakani Januari 20, mwakani, wakati akifanya kampeni, pamoja na mambo mengine aliahidi kuiondoa Marekani kutoka makubaliano hayo, akidai yanapora ajira na viwanda vya taifa lao.

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, aliwaambia wanahabari juzi kuwa mkataba huo wa TTP hautakuwa na maana bila ya Marekani.

Hata hivyo, mkataba huo uliotiwa saini Februari mwaka huu, ukiwa ni msingi wa sera ya biashara ya Rais Barack Obama, baada ya miaka saba ya mazungumzo bado haujaanza kutumika.

Trump alisema badala ya mkataba huo, kitu muhimu ni kurudisha ajira na viwanda na kuendeleza mpango wa kulinda miundombinu muhimu.

Ameahidi kuondoa vizuizi kuhusu sekta ya makaa ya mawe, ikiwamo masharti ya kiserikali ‘yanayoua’ uzalishaji wa nishati hiyo na pia kuzuia watu kutumia vibaya sheria ya visa.

Hata hivyo, hakugusia ahadi yake ya kubatilisha mpango wa huduma ya bima ya afya maarufu kama Obamacare na mpango wa kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ili kuzuia wahamiaji kutoka taifa hilo jirani.

Wakati huo huo, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Downing Street, imejibu tamko la Trump linalompigia chapuo kiongozi wa mpito wa Chama cha UKIP, Nigel Farage kuwa balozi wa Uingereza nchini Marekani.

Trump alikuwa ameandika kwenye Twitter kuwa ‘watu wengi’ wangependa kumwona Farage kama balozi na atafanya kazi ‘njema’.

Lakini Downing Street imesema: “Hakuna nafasi ya kazi kwa ajili hiyo. Tayari tuna balozi mzuri nchini Marekani.”

Farage aliyemuunga mkono Trump wakati wa kampeni za uchaguzi, alisema tamko hilo hakulitarajia, lakini aliongezea: “Iwapo ningekuwa na uwezo wa kuisaidia Uingereza kwa njia yoyote ile ningefanya.”

Kiongozi huyo mtata nchini Uingereza, alikuwa mwanasiasa wa kwanza Mwingereza kukutana na Trump baada ya ushindi wake.

Kiongozi wa Chama cha Liberal Democrat, Tim Farron, alichapisha kwenye mtandao wa Twitter, ujumbe kuwa pendekezo la kumtuma Farage kama balozi wa Uingereza nchini Marekani ‘ni hatua ya kijinga’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles