26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

KUHARA: UGONJWA UNAOWATESA ZAIDI WATOTO

Na MWANDISHI WETU,

MIONGONI mwa magonjwa ambayo huwasumbua watoto mara kwa mara ni kuhara. Lakini habari njema ni kwamba ugonjwa huu humalizika ndani ya siku chache iwapo mtoto atapohudumiwa vyema. Pamoja na hayo, ni vyema kujua jinsi ya kumsaidia mtoto anayekabiliana na ugonjwa huu na jinsi ya kuwakinga wale wasio na ugonjwa.

Chanzo cha ugonjwa wa kuhara

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema kuhara ni ugonjwa unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na virusi, lakini pia inaweza kuwa bakteria au vimelea vinginevyo vya magonjwa. Mgonjwa hupata choo cha majimaji mara nyingi.

Aina ya vimelea vinavyosababisha kuhara kwa watoto hutegemea eneo la kijiografia kulingana na viwango vya usafi wa mazingira, hali ya kiuchumi na usafi wa mwili.

Katika nchi zinazoendelea ambapo hali ya usafi wa mazingira ni duni na maeneo ambayo kinyesi cha binadamu hutumika kama mbolea, hukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuhara mara kwa mara kwa sababu taka hizi zitokanazo na binadamu ni rahisi kuingia katika vyakula na maji ya kunywa.

Kwa ujumla, vimelea vinavyosababisha kuhara ni rahisi kuambukiza kutoka mtu mmoja hadi mwingine au mtu kupata  ugonjwa kwa kujigusa na mazingira yaliyo na vimelea vya ugonjwa huu. Maambukizi yanayosababisha ugonjwa wa kuhara yanaweza kusambazwa kupitia:

Mikono michafu iliyoshika sehemu zenye vimelea vya ugonjwa, maji machafu au chakula kilichoingia vimelea vya ugonjwa. Wanyama wa kufugwa nyumbani, kujigusa katika mazingira yaliyochafuliwa na kinyesi cha binadamu na wadudu warukao na watambaao kama inzi na mende.

Virusi ni sababu kuu ya ugonjwa wa kuhara kwa watoto (hujulikana wakati mwingine kama ‘mafua ya tumbo’ ambayo yanaweza pia kusababisha kutapika). Kuna aina tofauti tofauti ya virusi vinavyosabisha kuhara kwa watoto, ambavyo husambazwa majumbani, shuleni na hata watoto wanapocheza na watoto wenzao.

Ugonjwa huu huwaathiri zaidi watoto wachanga ambao hawawezi kunywa maji mara kwa mara na wanapata upungufu wa maji mwilini (kwa kitaaalamu -dehydration).

Kundi la virusi lijulikanalo kama ‘Rotavirus’ ndilo linahusika zaidi na magonjwa ya kuhara kwa watoto. Virusi hawa husababisha mtoto kuhara choo cha maji maji mara kwa mara ingawa si watoto wote huonyesha dalili.

Kundi jingine ni la virusi wanaoitwa ‘coxsackievirus’ ambalo husababisha kuhara kwa watoto, lakini si sana ukilinganisha na kundi lililotangulia.

Pia kuhara kwa watoto kunaweza kusababishwa na uambukizi wa bakteria tofauti ambao kitaalamu wanaitwa Escherichia coli, Salmonella enteritis, Shigella, Giardia na Cryptosporidium.

Uambukizi wa magonjwa ya kuhara ni kawaida kuwakumba watoto walio wengi, lakini pia kuhara kunaweza kuwa dalili ya magonjwa mengine yasiyo ya uambukizi, mfano kuhara kunaweza kuashiria mzio (allergy), tumbo la mtoto linaposhindwa kumeng’enya maziwa (kwa kitaalamu-lactose intolerance) hususani anapobadilishiwa maziwa, kutoka maziwa ya mama na kutumia maziwa ya ng’ombe.

Dalili za ugonjwa wa kuhara kwa watoto

Dalili za ugonjwa huu huanza na tumbo kunyonga na hufuatiwa na kuhara ambako hudumu  kwa siku chache. Uambukizi wa virusi au bakteria wasababishao kuhara unaweza kusababisha pia mtoto kupata homa, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, kupungua uzito na upungufu wa maji mwilini.

Njia za kujikinga

Huwa ni vigumu mno kuwakinga watoto wasipate maambukizi yanayosababisha ugonjwa wa kuhara, zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitazosaidia kumkinga mwanao kupata maradhi ya tumbo.

Kwanza kabisa hakikisha watoto wananawa mikono vyema kwa maji safi na sabuni mara kwa mara, hususani baada ya kutoka chooni au kabla ya kula.

Kunawa mikono ni njia iliyo thabiti katika kuwakinga watoto na maambukizi yanayosababisha kuhara na ambayo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Mikono michafu hubeba vimelea vya magonjwa na watoto hupenda kung’ata na kunyonya vidole, kula kwa kutumia mikono au kuingiza kiganja mdomoni. Hakikisha vyoo na bafu nyumbani kwako viko katika hali ya usafi ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya magonjwa.

Osha matunda na mbogamboga kwa kutumia maji safi kabla ya kula, kwa sababu maji na chakula huweza kubeba vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa ya kuhara.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Tovuti ya Sayansi ya Afya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles