27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

MAJESHI MYANMAR YANAVYOENDELEZA MATESO KWA WAROHINGYA

NA JOSEPH HIZA,

MAJESHI ya Myanmar yanaendesha vita ya kikatili ya uuaji, ubakaji na mateso dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine, ripoti mpya ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (HRW) iliyotolewa Ijumaa iliyopita inasema.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini New York, Marekani linasema, Jeshi la Myanmar na walinzi wa mpakani walishiriki katika ubakaji wa kimakundi na mashambulizi ya kingono katika vijiji visivyopungua tisa katika Wilaya ya Maungdaw.

Matukio hayo ya kutisha yalitokea kuanzia Oktoba 9, hadi katikati ya Desemba 2016.

Kwa mujibu wa ripoti ya timu ya uchunguzi ya shirika hilo, wasichana hadi wenye umri wa chini ya miaka 13 walibakwa katika kampeni ya makusudi ya wanajeshi na askari polisi.

Ripoti hiyo imekuja baada ya kukusanya ushahidi wa matukio 28 tofauti ya mashambulizi ya kingono, ikiwamo mahojiano na wanawake tisa walioeleza kubakwa au kubakwa kimakundi chini ya mtutu wa bunduki na vikosi vya usalama wakati wa kile kinachoitwa ‘operesheni safisha’ kaskazini mwa jimbo la Rakhine.

Taarifa za mashuhuda kwa mujibu wa ripoti hiyo, inaeleza kwa muhtasari kiwango cha machafuko, ikiwamo watu kuteketezwa moto wakiwa hai, ubakaji wasichana wenye umri chini ya miaka 13 hadi kukata koo watoto wadogo hadi chini ya miaka mitano.

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imethibitisha ripoti hiyo, ikisema uchunguzi wake pia umeonesha kuwapo wazi kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Aye Aye Soe, msemaji wa Serikali ya Myanmar anasema Serikali imeiona ripoti hiyo na inasikitishwa na tuhuma hizo.

“Tume ya Uchunguzi inayoongozwa na ofisi ya Makamu wa Rais italichunguza hili. Iwapo ushahidi wa ukiukaji wa haki za binadamu utapatikana tutachukua hatua kali dhidi ya wahusika,” alidai.

Timu za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Bangladesh zilihoji Waislamu 220 wa jamii ya Rohingya waliokimbia jimbo hilo la Rakhine baada ya kuibuka kwa machafuko Oktoba mwaka jana.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu 69,000 wameikimbia Myanmar kuelekea Bangladesh tangu machafuko yalipoanza mwaka jana.

Kati ya watu 220 waliohojiwa, asilimia 65 walishuhudia mauaji huku nusu wakishuhudia wanafamilia wao wakiuawa.

Mwammke mmoja wa Kijiji cha Kyet Yoe Pyin anaeleza namna ambavyo bintiye mwenye umri wa miaka mitano alivyouawa wakati akijaribu kuwazuia washambuliaji wasimbake mama yake.

“Mtoto wa watu alikuwa akipiga kelele, kuona hivyo, mmoja wa wabakaji hao akachukua kisu kirefu na kumuua kwa kumkata koo kana kwamba anachinja kuku,” ripoti inaeleza.

Aidha, msichana mmoja mdogo mdogo anaeleza kwa timu ya uchunguzi ya UN kuwa askari walimuua baba yake kisha wakambaka mama yake kabla ya kumfungia ndani ya nyumba waliyoiteketeza kwa moto.

“Yote haya yalitokea mbele ya macho yangu,” anasema.

Mkimbizi mmoja wa Rohingya, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mohammed naye alimpoteza mwanae mwenye umri wa miezi 17 wakati akiwakimbia wanajeshi.

Mohammed anasema alikimbia wakati wanajeshi walipoanza kushambulia vijiji vyao, wakiwateketeza kwa moto babu na bibi yake wakiwa hai.

“Tusingeweza kubaki nyumbani, tulikimbia na kwenda mafichoni na katika mazingira haya tulipotelewa na mtoto,” anasema.

Serikali ya Myanmar mara kwa mara imekuwa ikikana madai ya ukiukaji wa haki za binadamu ikisema wanaendesha ‘operesheni safisha’ dhidi ya washukiwa wa mashambulizi dhidi ya walinzi wa mpakani yaliyotokea Oktoba 2016.

Hilo ni shambulio lililofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya kituo cha ulinzi wa mpakani mwa Myanmar na Bangladesh.

Wadadisi wa mambo wanalieleza shambulio hilo limekuwa kisingizio cha jeshi na waumini wenye msimamo mkali wa Budha kuwalenga Waislamu wa Rohingya, ambayo ni jamii ya walio wachache nchini humo.

Viongozi wa eneo hilo na Buddha wanawatuhumu Waislamu hao kuhusiana na shambulio hilo, ambapo askari tisa wa jeshi la Myanmar waliuawa.

Shambulio hilo liliibua Operesheni hiyo safisha, iliyoshuhudia Warohingya 20 wakiuliwa katika siku ya kwanza kwa kupigwa risasi kutokea nyuma wakiwa hawana silaha, ripoti ambayo hata hivyo serikali imeikana.

Hata hivyo, Serikali ya Myanmar imekuwa ikiweka vikwazo kwa mashirika ya misaada na waandishi wa habari kufika eneo hilo lenye Waislamu milioni 1.3.

Mkoa wa Rakhine unaopatikana kaskazini magharibi mwa Myanmar wanakoishi Waislamu wengi, tangu mwaka 2012 umekuwa ukiathiriwa na vitendo vya utumiaji mabavu na ubaguzi vinavyofanywa na waumini wa Buddha wenye misimamo mikali.

Zaidi ya Warohingya 300,000 wamekuwa wakiishi nchini Bangladesh kwa miongo kadhaa ukiondoa wale 69,000 waliovuka mpaka tangu Oktoba mwaka jana wakati machafuko yalipoibuka upya.

Vurugu hizo zilisababisha ukosoaji wa kimataifa dhidi ya Myanmar, huku Bangladesh ikihangaika kuwahifadhi Warohingya waliovuka mpaka.

Serikali ya Bangladesh kwa sasa inapanga kuwahamishia katika kisiwa kisichokaliwa na watu cha Thengar Char, mpango ambao hata hivyo umezusha wasiwasi miongoni mwa Warohingya na baadhi ya makundi ya haki za binadamu na UN kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Bangladesh Mahmood Ali aliwaarifu juu ya mpango huo, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika wapatao 60 yakiwamo ya UN na kuomba msaada wao kuwahamisha Warohingya hao kutoka kambi zilizofurika katika Wilaya ya Cox Bazar kwenda kisiwa hicho hatari kilichoko kusini-mashariki mwa Bangladesh.

Maafisa wa serikali wamesema tayari serikali inapima eneo hilo.

Waziri Ali aliwaambia wanadiplomasia kuwa idadi kubwa ya wakimbizi inafanya iwe vigumu kwa serikali kutoa msaada wa kutosha na imesababisha matatizo ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kiusalama.

Hata hivyo, Kisiwa cha Thengar Char ndiyo mlango wa Mto Meghna na kilitoka baharini miaka minane tu iliyopita na hufurika kila inapotokea dhoruba kubwa.

Lakini badala ya kupelekwa katika kiswani hicho, Warohingya wameiomba jamii ya kimataifa kuwasaidia kuishinikiza Serikali ya Myanmar iwarejeshee uraia wao.

"Hatutaki kuishi Bangladesh kwa muda mrefu, tunataka kurudi kwetu Myanmar, lakini serikali ya Burma ilifuta uraia wetu, hivyo tunauomba UN utusaidie kuishinikiza serikali hiyo ili turejeshewe uraia wetu," alisema Mohammad Younus mmoja wa wakimbizi hao.

"Na wakati tunapoendelea kuishi Bangladesh, tunaomba tutendewe kama binadamu ili tupate makazi mazuri, chakula, matibabu yanayostahiki na elimu. Tunataka kujenga jamii iliyelimika na tunaomba jamii ya kimataifa itusaidie."

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles