Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’, Sebastian Nkoma, amesema kuwa anatarajia kikosi chake kitapunguza idadi ya mabao ya kufungwa kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Nigeria, Jumapili Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Nkoma alisema kikosi chake kilipata kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Nigeria katika mchezo wa awali kutokana na ugeni wa mashindano ya kimataifa.
Alisema hivi sasa timu yake imefanikiwa kufanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza, hivyo matumaini yake ni kupunguza idadi ya mabao waliyofungwa na Nigeria.
“Tumejipanga katika mchezo wa marudiano tupunguze idadi ya mabao ya kufungwa au tushinde, kule Nigeria wenzetu wana uzoefu wa muda mrefu sana tofauti na sisi,” alisema.
“Mpira ni mchezo wa makosa, unapokosea unajifunza, hivyo nikiwa kama mwalimu nimejitahidi kwa uwezo wangu kukijenga kikosi changu na kuwaondoa hofu wachezaji,” alisema Nkoma.
Nkoma alisema Nigeria wana kikosi kizuri, ambacho kimeandaliwa kwa muda mrefu na kucheza mechi mbalimbali za kimataifa tofauti na Tanzania.
Mara baada ya kurejea, kocha mkuu wa timu hiyo, Nkoma, amesema walipoteza mchezo wa awali kwa kufungwa mabao 3-0 kwa sababu Nigeria ni timu bora na Tanzanite kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.