Na HERIETH FAUSTINE,
KITUNGUU swaumu ni jamii ya vitunguu ambavyo kwa kitaalamu huitwa Allium Sativum ambapo hutegemewa katika kuongeza ladha nzuri kwenye vyakula mbalimbali.
Licha ya kutumika wakati wa kupika na kunogesha vyakula, wataalamu wa tiba asili wanasema ni dawa endapo kitatumika vizuri.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kitunguu swaumu kimeonekana kuwa na uwezo wa kutibu maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali.
Aidha, husaidia kuzuia magonjwa ya moyo ikiwamo kuondoa ‘cholesterol’ katika mishipa ya damu na hivyo kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu.
Pia hutibu saratani ya tumbo na utumbo mkubwa, tafiti zinaonyesha kuna nchi zina idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani kutokana na wakazi wake kuwa na utamaduni wa kutumia vitunguu kwa wingi.
Kitunguu swaumu ni tiba nzuri ya magonjwa ya ngozi yenye vilenge lenge ambapo dalili zake ni madoa meupe yenye magamba ambayo huchunika kama ngozi iliyoungua mikononi, miguuni, shingoni au usoni kwa kukitwanga na kukipaka katika sehemu hizo.
Kitunguu swaumu pia hutibu aina mbalimbali za tambaza kama ya misuli, viungo pamoja na wale watu wenye matatizo ya kupata choo kwa muda wa siku mbili au zaidi.
Aidha, pia inasaidia kwa wenye matatizo ya pumu na kubanwa katika mapafu pamoja na kushindwa kupumua ghafla, hata ukiumwa na nge unaweza kusaga kitunguu na kubandika pale ulipoumwa.
Vitunguu swaumu husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu, hata hivyo inashauriwa wagonjwa wa kisukari wanaotumia insulin wasitumie kitunguu swaumu kwa wingi.
Vile vile kitunguu swaumu hutibu kuharisha pamoja na mishipa iliyovimba ambayo hujikunja na hivyo kusababisha maumivu makali, na wakati mwingine mishipa hiyo huonekana katika miguu ya watu wa makamo na wajawazito.
Kitunguu swaumu kimekuwa kikitumika kutibu na kuboresha afya ya mwili na kumfanya mtumiaji awe mrembo na mwenye afya bora.
Wataalamu wanashauri kitunguu swaumu kuliwa kibichi kila siku kwa ni husaidia kuboresha afya ya muhusika.