HIVI karibuni Rais mstaaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alikaririwa akishauri Kiswahili kitumike kama lugha rasmi ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.
Alisema hilo litawawezesha wanafunzi kufaulu vizuri masomo yao kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha wanayoielewa.
Rais huyo mstaafu alisema ifike wakati sasa mwanafunzi anapoanza shule ya msingi hadi anamaliza chuo kikuu awe anatumia Kiswahili, hata kufikia ngazi ya profesa, na lugha nyingine zifundishwe kama lugha tu.
Si siri kwamba mjadala huo wa kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia kwa ngazi zote, au la, umekuwapo kwa miongo mingi – tangu wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.
Na bahati mbaya hadi sasa hakujawa na utashi wa kutosha au uamuzi madhubuti wa kulitekeleza hilo.
Wako wanaounga mkono hoja hiyo (kama alivyo Mwinyi) na wako wanaoipinga wakidai pamoja na mambo mengine, kwamba kufanya hivyo kutazidi kudidimiza elimu nchini, kwamba Tanzania itazidi kurudi nyuma katika ushindani wa maendeleo ya elimu duniani.
Vilevile wanahitimisha kwa kudai kwamba Kiswahili hakijajitosheleza katika maneno kama ilivyo kwa lugha kama Kiingereza!
Lakini wenye mtazamo huo wanakataa (wanashindwa) kutambua jinsi matumizi ya lugha inayoeleweka na watu wengi katika kufundishia kwa ngazi zote, inavyochangia kuharakisha maendeleo katika nchi husika. Mifano iko wazi na mingi – China, Urusi, Ufaransa, Ujerumani, Italia na nchi nyingine nyingi.
Kwa sababu hiyo, wenye msimamo wa kupinga Kiswahili kutumika katika ngazi zote za elimu wana hoja ambayo si madhubuti na ina matege.
Ukweli ni kwamba wenye msimamo huo wanatawaliwa na kasumba ya ukoloni, kutojiamini na mtazamo wenye makengeza. Ndiyo sababu hivi sasa Tanzania iko hatarini kupoteza hadhi yake ya kuwa kinara wa Kiswahili duniani!
Wakati wa uongozi wa Mwalimu, ulipitishwa uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi ya shule ya msingi.
Wanaopinga Kiswahili kufundishwa katika ngazi zote za elimu wanatoa mfano jinsi wanafunzi wanavyopata tabu ya kuelewa masomo wanapojiunga elimu ya sekondari.
Hiyo ni kweli, lakini jambo hilo linatokana na uamuzi nusu nusu uliofanywa wakati huo – zikiwamo juhudi zinazofanywa kuhakikisha hata mfumo huo unafutwa!
Tunachosema ni kwamba ikiwa tangu wakati huo ungetolewa uamuzi madhubuti wa kuhakikisha Kiswahili kinafundishwa katika ngazi zote, hali isingekuwa kama ilivyo hivi sasa.
Ni kwamba hatua hiyo ingeambatana na kufanyika juhudi za kila aina na kila mdau, wakiwamo viongozi na watendaji kuhakikisha azma hiyo inatekelezwa.
Ndiyo sababu tunasema kuna haja kwa Tanzania kurejesha heshima yake ya kuwa kinara wa Kiswahili duniani. Viongozi na watendaji waache tabia waliyonayo ya kukinyanyapaa na kukionea aibu Kiswahili katika nyanja ya kimataifa.
Hatua madhubuti na za pamoja zichukuliwe kuhakikisha Kiswahili kinafundishwa katika ngazi zote za elimu, kusaidia na kuchangia kuharakisha maendeleo ya taifa na wananchi wake kwa ujumla.