30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kilimo, uvuvi vyaundiwa dawati maalumu

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amezindua Dawati la Sekta Binafsi, ikiwa ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli ya kuleta mageuzi katika sekta za mifugo na uvuvu ili kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa.

Akizindua Dawati hilo jijini hapa juzi, Waziri Mpina alisema ni matarajio ya serikali ni kuona dawati linakuwa ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi na kuchangia ipasavyo ukuaji na maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

“Dawati hili maalumu linajumuisha wadau wote katika sekta hizi, litashughulikia kero na usumbufu wanaokutana nao wadau na kushindwa kutoa mchango stahiki katika uchumi wa taifa.

“Tanzania imebahatika kuwa na raslimali nyingi za mifugo na uvuvi ambazo kwa mwaka 2017 zilichangia asilimia 6.9 kwa mifugo na asilimia 2.2 kwa uvuvi kwenye pato la taifa,” alisema na kuongeza kuwa asilimia hizo  katika pato la taifa ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya mifugo iliyopo.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza dawati hilo lifanye kazi kwa bidii, uadilifu na kuweka uzalendo mbele, ili liwe mfano wa utendaji kwa kuainisha fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta na kuifanya Tanzania iwe katika nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara.

“Tanzania inakadiriwa kuwa na ng’ombe wapatao milioni 30.5 na kuifanya nchi yetu kuwa ya pili Barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe. Pamoja na idadi hiyo kubwa bado haijabadilisha maisha watu,” alisema.

Waziri Mpina alisema kupitia Dawati la Sekta Binafsi, kero, ukiritimba uliokuwa unakwamisha maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi ambayo imeajiri zaidi ya kaya milioni sita ya Watanzania  zinatokomezwa na kuleta matokeo chanya.

Alisema mwaka 2017 Tanzania ilikuwa na mbuzi milioni 10.8, kondoo milioni 5.3, kuku wa asili walikuwa milioni 38.2, kuku wa kisasa milioni 36.6, nguruwe milioni 1.9 na punda wapatao 595,160.

Akizungumzia uvuvi, waziri Mpina alisema Tanzania imebarikiwa kuwana rasilimali nyingi ambazo zimegawanyika kulingana na mifumo ya kiikolojia. Kwa upande wa Ukanda wa Bahari Kuu (Exclusive Economic Zone) lina ukubwa wa kilomita za mraba 223,000.

Mbali ya kuishukuru Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Waziri Mpina alizishukuru pia Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ASPIRES, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Shirika la Misaada na Maendeleo la Maendeleo la Marekani (USAID) kwa kufanikisha uundwaji wa dawati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles