Na TIMOTHY ITEMBE-TARIME
NYAMOHANGA Suguta (75) mkazi wa Kitongoji cha Kibeyo Kijiji cha Getenga Kata ya Mbogi wilayani Tarime, amejiunga na darasa la kwanza mwaka huu katika shule mpya ya msingi ya Makerero baada ya kuamua kusoma.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Riziki Focus, alisema mwanafunzi huyo amejiunga na darasa la kwanza kutokana na kufanya vizuri katika darasa la utayari kwa masomo yake ya kazi za mikono, hesabu na mwandiko.
Akizungumza katika uzinduzi wa shule hiyo juzi, Focus alisema mwanafunzi huyo aliandikishwa darasa hilo mwaka huu katika Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (Memkwa).
“Mzee huyu alianza mwaka jana kwa kusoma darasa la awali na alifanya vema masomo yake ya darasa hilo.
“Tumeamua kumwandikisha darasa la kwanza katika mpango wa Memkwa na anahudhuria vizuri shuleni hapa kila siku tena kwa bidii sana,” alisema.
Shule ya Msingi Makerero ilifunguliwa Februari mosi mwaka huu na Kaimu Ofisa Elimu Msingi, Tumaini Musoma kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Apoo Tindwa.
Ilianzishwa Desemba 30, mwaka jana ikiwa na mwalimu mmoja wa darasa la kwanza na mmoja wa darasa la utayari.
Hivi sasa ina wanafunzi 66 wa darasa la kwanza akiwamo Suguta wakati wa awali wakiwa 46.
Naye Mwalimu Magreth Albinus ambaye alimfundisha Suguta darasa la awali, alisema kufanya vizuri kwa kikongwe huyo kunatokana na kujituma na nia yake ya dhati ya kutaka kujua kusoma na kuandika.
“Mzee huyo alijiunga na elimu ya awalii mwaka jana na kuendelea muda wote kuhudhuria masomo na kila kazi za shuleni.
“Awali nilimuonea aibu lakini kila nilipokuwa nikimuelekeza anatekeleza maagizo yangu hivyo nilimteua kuwa kiranja kusimamia wenzake, alifanya vizuri,” alisema Magreth.
Akielezea uamuzi wake wa kujiunga na shule, Suguta alisema kufanya hivyo baada ya kuvutiwa na elimu.
Suguta alisema aliwahi kusoma na kukomea darasa la pili mwaka 1950 kutokana na kukumbwa na mazingira magumu na kulazimishwa kuchunga mifugo na kulima na familia yake.
Alisema aliona ajiunge na elimu ya msingi ikiwa ni kutimiza malengo yake ya kupata elimu na kuhitimu na amekuwa na kiu kubwa ya kujua hesabu na kuandika Kiswahili na Kiingereza ambavyo vitamfaa kwa shughuli zake za kila siku.
Diwani Kata ya Mbogi, Ezekiel Matiko (Chadema) alisema shule hiyo ilijengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na mchango wa mabati na saruji mifuko 20 na madawati 20 kutoka halmashauri.
Aliomba waongezwe walimu wengine watatu ili iwe na walimu wanne na watakaokidhi masomo na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wake.