30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JEN. MABEYO MKUU MPYA WA MAJESHI

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amemteua Luteni Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.

Pamoja na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Luteni Jenerali Mabeyo amepandishwa cheo na kuwa Jenerali.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kwamba Jenerali Mabeyo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange, ambaye amestaafu kazi Januari 31, mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Meja Jenerali James Mwakibolwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.

Pamoja na kuteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Meja Jenerali James Mwakibolwa amepandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali.

Luteni Jenerali James Mwakibolwa anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Venance  Mabeyo, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.

“Uteuzi huu unaanza mara moja na tarehe ya kuapishwa itatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa hiyo.

Januari 30, mwaka jana Rais Dk. John Magufuli , alimuongezea muda wa mwaka mmoja Mkuu wa  Majeshi ya Ulinzi nchini,Jenerali David Mwamunyange, ambaye amekamilisha muda wake Januari 31, mwaka huu kwa mujibu wa katiba na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari mwaka jana katika Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyopo  Upanga jijini Dar es salaam, Jenerali Mstaafu Mwamunyange alisema alitakiwa kuungana na Brigedia wanne wa Jeshi la ulinzi nchini  pamoja na Meneja Jenerali  wawili  ambapo wote walistaafu mwaka jana.

 “Mimi mwenyewe ilikuwa nistaafu kazi leo tarehe 30 Januari 2016, lakini Rais na Amri Jeshi Mkuu ameamua kunibakiza katika utumishi jeshini kwa mwaka mmoja kuazia leo Januari 30, 2016 hadi Januari 31, 2017,” alisema Jenerali Mwamunyange

Akitaja sababu iliyomfanya Rais Magufuli kumuongezea muda huo imetokana na Rais kutopata mtu sahihi wa kujaza nafasi hiyo aliyonayo .

Hata hivyo, Jenerali Mwamunyange alisema Rais Magufuli amemteua  Luteni Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi.

Pamoja na hilo pia Rais Dk. Magufuli alifanya uteuzi mkubwa ndani ya Jeshi hilo wa nyadhifa mbalimbali.

 Walioteuliwa mwaka jana na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dk. Magufuli  ni Meja Jenerali James Mwakibolwa  kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la nchi Kavu, ambaye alichukua nafasi ya Meja Jenerali Salum Kijuu aliyestaaafu kazi mwaka jana baada ya kufikisha umri wa kustaafu kisheria. Kabla ya uteuzi huo, Meja Mwakibolwa alikuwa ni Mkuu wa Tawi la Utendaji wa Kivita na Mafunzo Makao Makuu ya Jeshi.

Jeneral Mwamunyange alimtaja pia Kamanda mwingine aliyeteuliwa na Rais ni Meja Jenerali Yakub Sirakwi kuwa  Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (Commandant NDC) kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Gaudence Milanzi ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasilia na Utalii, nafasi ambayo anahudumu nayo. Meja Jenerali Sirakwi alikuwa Mratibu Msaidizi Mkuu Baraza la Usalama wa Taifa- BUT.

Mwingine  aliyeteuliwa  na Rais Magufuli ni Brigedia Jenerali George William Ingram kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga akichukua nafasi ya  Meja Jenerali Joseph  Pwani aliyestaafu Januari 31, mwaka huo kwa mujibu wa sheria.

Brigeda Jenerali Ingram alikuwa Ofisa Mnadhimu katika Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Anga.

Safari ya Mabeyo

Septemba 12, mwaka 2014 Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alimpandisha cheo Venance Mabeyo kutoka Brigedia Jenerali kuwa Meja Jenerali.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa huenda ndiyo ilikuwa ni mwanzo wa kuelekea kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, ambayo ilitimia jana kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya nchi.

Kikwete ambaye pia alikuwa Amiri Jeshi Mkuu kwa wakati huo alimteua Mabeyo kwa mujibu wa Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Aya ya 7.01 Kifungu cha (3).

Mbali naye pia aliwapandisha  cheo kuwa Meja Jenerali  maofisa wengine sita, ambao ni  Brigedia Jenerali Gaudence Milanzi, Jenerali Mwakibolwa, Ndetaulwa Zakayo,  Simon Mumwi, Issa Nassor, Rogastian Laswai.

Wote hao walivishwa vyeo hivyo na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange kwa niaba ya Rais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles